Habari za Kitaifa

Historia yakaribia kuandikwa Oduor, Askul wakipitishwa na Kamati ya Bunge

Na CHARLES WASONGA August 14th, 2024 1 min read

KAMATI ya Bunge la Kitaifa kuhusu Uteuzi imependekeza kuwa Dorcas Agik Odhong Oduor kwa uteuzi rasmi kuwa Mwanasheria Mkuu nchini.

Aidha, Kamati hiyo inayoongozwa na Spika wa Bunge hilo Moses Wetang’ula imebaini kuwa Bi Beatrice Askul Moe anafaa kuhudumu kama Waziri wa Masuala ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Maendeleo ya Kikanda na Maendeleo ya Maeneo Kame.

Hii ni kulingana na ripoti ya kamati hiyo ya wanachama 20, iliyowasilishwa katika bunge la kitaifa Jumatano, Agosti 14, 2024, saa nane na nusu alasiri.

“Kwa mujibu wa matokeo ya Kamati ya Bunge hili Kuhusu Uteuzi kuhusiana na kupigwa msasa kwa wateule waliopendekezwa kuwa Waziri wa Masuala ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na Maendeleo ya Kanda na Mwanasheria Mkuu wa Jamhuri ya Kenya, ripoti iliyowasilishwa bungeni leo Agosti 14, 2024, Bunge hili linaidhinisha uteuzi wa watu hawa; Bi Beatrice Askul Moe kuwa Waziri wa Masuala ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na Maendeleo ya Kikanda na Dorcas Agik Odhong Oduor kuwa Mwanasheria Mkuu wa Jamhuri ya Kenya,” ikasema hoja kuhusu ripoti ya kamati hiyo.

Endapo ripoti hiyo itaidhinishwa na kamati ya bunge lote, historia itaandikishwa nchini Kenya.

Bi Oduor atakuwa mwanamke wa kwanza kushikilia wadhifa wa Mwanasheria Mkuu tangu Kenya ilipate uhuru. Aidha, Bi Moe ataingia katika mabuku ya historia kama mwanamke wa kwanza kutoka Jamii ya Waturkana kushikilia washifa wa Uwaziri katika serikali ya kitaifa.