Mkahawa mchafu jijini Nairobi wafungwa
AFISA Mkuu wa Mazingira Kaunti ya Nairobi Bw Geoffrey Mosiria amefunga hoteli moja jijini kwa kukosa kudumisha viwango hitajika vya usafi.
Mkahawa huo huandaa vyakula kama vile mayai, kebab na smokies ambavyo husambazwa kwa wachuuzi wa mitaani.
Kwenye mahojiano na Taifa Dijitali, Bw Mosiria alisema hatua ya kufunga mkahawa huo kwa muda usiojulikana ni kutokana na wafanyabiashara kukosa kurekebeisha mienendo baada ya kushtakiwa na kuachiliwa.
“Alikabidhiwa barua ya kufunga biashara. Unapowakamata na kuwafikisha mahakamani, wengi huachiliwa kwa dhamana. Baada ya kulipa dhamana hiyo wanarejea kuendeleza biashara bila kujali usafi,” alisema Bw Mosiria.
Bw Mosiria ameambia Taifa Leo kuwa mazingira yaliyokuwa yakitumika kuandaa chakula yanaweza yakasababisha magonjwa mbalimbali kwa wateja jijini Nairobi.
Alibainisha kuwa maafisa wa kaunti walifanya ukaguzi wa ghafla siku chache zilizopita na kumuonya mmiliki huyo pamoja na kumpa amri kufunga kwa siku tatu ili kudumisha usafi kabla ya kufunguliwa tena.
Hata hivyo, maafisa hao walipigwa na butwaa baada ya kurejea na kupata hali haijabadilika hata baada ya kumuamrisha kufanya usafi kwenye duka lake.
“Maafisa wa mazingira walifika mkahawani humo na kupata sehemu yakuandalia mapishi ni chafu. Walizungumza na mmiliki wa sehemu hiyo na kumwelekeza asafishe kwa kuwa kazi yetu si kufunga biashara ila kuangalia kiwango cha usafi kinachodumishwa,” alieleza Bw Mosiria.
“Maafisa wangu walimpa barua ya kwanza ya kufunga kwa siku tatu ili kufanya usafi kwa sababu mkahawa huo ulikuwa ukipata wateja wengi. Alikubali ombi letu, lakini tuliporudi Ijumaa Agosti 16, tulipata hali haijabadilika ,” aliongeza Bw Mosiria.
Aliwataka wafanyabiashara wengine wanaojishughulisha na chakula kuhakikisha wanazingatia viwango vya usafi.