Michezo

Drama Ajax wakilemea Panathinaikos baada ya penalti 34!

Na MASHIRIKA August 17th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

AJAX walikomoa Panathinaikos kwa njia ya penalti 13-12 baada ya drama katika upigaji penalti kwenye mechi ya kuingia awamu ya muondoano ya Ligi ya Uropa ugani Johan Cruyff mnamo Alhamisi.

Jumla ya penalti 34 za kuamua mshindi zilipigwa katika mechi ya marudiano baada ya kila mmoja kushinda ugenini 1-0.Kipa Remko Pasveer, 40, alipangua penalti tano za Panathinaikos. Naye difenda Anton Gaaei akapachika penalti ya ushindi ya Ajax.

Ajax walitwaa tiketi ya kuvaana na Jagiellonia Bialystok (Poland) katika muondoano wa kuingia makundi ya Ligi ya Uropa licha ya mshambulizi Brian Brobbey kupoteza penalti mbili nao Bertrand Traore na Youri Baas pia walipiga penalti fyongo.

Kocha Francesco Farioli alisema shughuli ya kupiga penalti za kuamua mshindi, ambayo ilidumu dakika 25, ilikuwa ya ajabu sana.

“Moyo wa timu na kujitolea kwake ulikuwa katika kiwango kingine. Hatuko imara, lakini hatuwezi kusema kuwa wachezaji hawakujituma kwa moyo wao wote,” akasema Farioli.

Idadi hiyo ya penalti ni ya pili kwa wingi katika mashindano yoyote ya Ulaya baada ya Glentoran kutoka Ireland Kaskazini kubanduliwa 14-13 na Gzira United (Malta) katika mechi za kufuzu za Europa Conference League msimu 2023-2024.

“Tunafurahia kupiga hatua moja muhimu mbele,” akasema Farioli.Mshindi kati ya Ajax na Jagiellonia Bialystok mnamo Agosti 22 na Agosti 29, ataingia makundi ya Ligi ya Uropa.

Mechi inayoshikilia rekodi ya dunia kwa penalti nyingi za kuamua mshindi ni kati ya timu za Israel, SC Dimona na Shimshon Tel Aviv mwezi Mei mwaka huu.

Dimona ilishinda 23-22 baada ya mikwaju 56 kuchotwa.