Akili MaliMakala

Akili ni mali: Kutoka uuzaji michoro ya nyumba hadi uuzaji wa nyumba

Na PETER CHANGTOEK August 18th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

ALIPOKUWA akifanya kazi katika kampuni moja ya kujenga na kuuza nyumba jijini Nairobi mwaka mmoja tu baada ya kufuzu chuoni, aliupata ujuzi ambao aliutumia baadaye kujijenga kimaisha.

Mary Diana, 29, ni Mkurugenzi Mtendaji na Mwanzilishi wa MD Modern Homes, kampuni inayohusika na uuzaji nyumba, ploti na mashamba.

Safari yake ya kuanzisha kampuni ya uuzaji wa nyumba ilianza mnamo 2018, mwaka mmoja tu, baada ya kufuzu katika Chuo Kikuu cha TUK.

“Nilianza kwa kuajiriwa kama muuzaji wa michoro ya nyumba na baadaye kuanza kutafuta mali kama nyumba ili kukidhi mahitaji ya wateja wangu,” asema Diana, mzawa wa tatu  katika familia ya watoto watano.

Baada ya muda, asema, kutokana na ubora wake kazini, alipanda ngazi hadi kuwa kiongozi wa timu yake ya wafanyakazi, kisha baadaye akawa meneja wa mauzo, nafasi ambayo iliwasilisha fursa ya kuimarisha ujuzi wake.

Mjasiriamali huyo anafichua kuwa, eneo lake la utaalamu ni uuzaji, kutafuta mali na kuuza kwenye hifadhidata ya wateja wake.

“Ninasukumwa na hamu ya kusaidia wateja kupata nyumba zilizo kwa ndoto zao. Kwa uzoefu wa zaidi ya miaka sita kutoka kwa ajira yangu ya awali na nikiwa MD Modern Homes, nimekuwa nikiwasaidia wateja kupata aina tofauti za nyumba wanazozitaka,” asema Diana, aliyeianzisha kampuni yake mwanzoni mwa 2022.

Mary Diana, mwasisi wa kampuni ya MD Modern Homes katika afisi yake, Nairobi. PICHA | PETER CHANGTOEK

Mwanzoni, alikuwa akiogopa kidogo kuacha ajira na kujitosa katika ujasiriamali na kulenga kuiboresha brandi yake, lakini baadaye aliamua kufanya hivyo, na sasa, kampuni yake inavuma.

“Lakini nashukuru kwa kuwa biashara ilikua vizuri na niliweza kupenya kwenye tasnia kutoka mwezi wa kwanza na sikurudi nyuma. Tunaendelea vizuri na tunamshukuru Mungu,” ongeza.

“Nilipoanza, nilitumia njia tofauti kuendesha matangazo kwenye majukwaa ya mitandao ya kijamii ili kupata mwonekano zaidi, na uundaji wa maudhui ya kidijitali kama, kama vile mabango na pia kuwezesha mchakato mzima wa umiliki wa nyumba, kuanzia wakati mtu anapotembelea tovuti hadi anapoimiliki nyumba rasmi,” aeleza mjasiriamali huyo.

Diana amepata tuzo nyingi tangu alipokuwa ameajiriwa, hadi wakati huu anapoiendesha kampuni yake. Alipata tuzo 2021, 2022, akiwa ameajiriwa, na  2023 na 2024, akiwa katika kampuni yake ya MD Modern Homes – kutoka kwa mashirika mbalimbali; kama vile KPRA, NABLA, miongoni mwa mengine.

Anasema kuwa, kuwashauri wafanyabiashara kadhaa wanaojiunga na tasnia hii kupitia mafunzo hadi waweze kufanya biashara peke yao, kunamfanya aridhike zaidi.

“Kuiga kwao kutoka kwangu, pia kunaniridhisha sana,” aongeza.

Anafichua kuwa, kampuni yake inashirikiana na wadau, wamiliki wa nyumba, wawekezaji – kampuni na watu binafsi ambao wana nyumba za kuuza au kukodisha na wanaonesha mali zao kwenye majukwaa ya MD Modern Homes, na kupata wanunuzi, hivyo kufanya iwe rahisi kwa wanunuzi kutambua mali wanazozitaka.

Anasema kuwa, asilimia 90 ya wateja wake hupatikana kupitia kwa majukwaa ya mitandao ya kijamii ya MD Modern Homes, ambapo ana wafuasi zaidi ya 70,000, na wana wafuasi wengi hadi wale walioko katika nje ya nchi.

Diana anasema kuwa, wao hutumia Facebook, YouTube, Instagram, LinkedIn, Twitter, TikTok. Pia, huwapata wateja kupitia kwa marejeleo kutoka kwa wateja walioridhika na huduma za kampuni hiyo.

Mjasiriamali huyo anasema kuwa, uaminifu, uwazi, na uwajibikaji, ni muhimu wakati mtu anafanya biashara.