Habari za Kaunti

Ombi wakazi wasichinje mbuzi waliopewa kama msaada

Na SIAGO CECE August 20th, 2024 1 min read

SERIKALI ya Kaunti ya Kwale imewasihi wakazi walionufaika na mpango wa kusambaza mbuzi wanaostahimili ukame, kutowachinja mifugo hao kabla wazaane.

Mpango huo wa kugawa mbuzi aina ya Galla uliwalenga watu wanaoishi na ulemavu.

Akizungumza eneo la Lunga Lunga alipogawa mbuzi 90, Naibu Gavana wa Kwale, Bw Chirema Kombo, alisema kaunti inataka kupunguza viwango vya umaskini kwa wakazi.

“Mabadiliko ya tabianchi ni changamoto ya kimataifa na inatuathiri sisi sote. Mifugo hii itaimarisha ustahimilivu dhidi ya changamoto za hali ya hewa na pia kuchochea mbinu endelevu za kilimo,” Bw Kombo alisema.

Mwenyekiti wa kikundi cha Maendeleo Disability, Nzingo Kombo, alisifu hatua ya kaunti hiyo kuwasaidia, akisema wengi wao hawawezi kujishughulisha na kilimo hivyo basi ufugaji wa mbuzi ni rahisi kwao kwani maeneo ya malisho na maji yanapatikana kwa urahisi.