Umri si hoja, Luka Modric, 39 ajumuishwa katika kikosi cha timu ya taifa ya Croatia
KIUNGO mahiri Luka Modric wa klabu ya Real Madrid, amejumuishwa katika kikosi cha wachezaji 24 wa timu ya taifa ya Croatia itakayoshiriki michuano ya UEFA Nations League, licha ya umri wake mkubwa.
Modric ambaye alisaini mkataba wa mwaka mmoja kuendelea kuchezea Madrid, ana umri wa miaka 39. Hata hivyo, kocha Zlatko Dalic, anaamini kwamba umri sio tatizo, huku akisisitiza kwamba nyota huyo angali na nguvu za kusaidia timu ya taifa baada ya kuzidi kutwaa tuzo za mchezaji bora katika mashindano mbalimbali.
Kiungo huyo mchezeshaji aliye kwenye orodha ya wachezaji wanaoongoza katika ufungaji mabao kwenye klabu ya Madrid, ndiye staa wa kutoa pasi za uhakika, hivyo mchango wake hauwezi kupuuzwa.
“Umri sio tatizo, bali kitu muhimu ni jinsi anavyocheza uwanjani na kusaidia timu. Bila shaka ataendelea kuwika kwa miaka mingi,” aliongeza kocha Dalic.
Modric amechezea Croatia mara 178 tangu apewe nafasi kwa mara ya kwanza mnamo 2006, alipokuwa na umri wa miaka 20. Tayari Domagoj Vida na Marcelo Brozovic wa rika lake wamestaafu kucheza soka ya kimataifa.
Croatia wamepangiwa katika Kundi A la Nations League ambapo wataanzia ugenini dhidi ya Ureno mnamo Septemba 5, kabla ya kualika Poland siku tatu baadaye.