Habari za Kitaifa

Oduor, Askul waapishwa rasmi na kuandikisha historia

Na CHARLES WASONGA August 20th, 2024 2 min read

BI Dorcas Agik Odhong Oduor Jumanne, Agosti 20, 2024 aliapishwa rasmi kuwa Mwanasheria Mkuu na kuandikisha historia kama mwanamke wa kwanza kushikilia wadhifa huo nchini.

Naye Bi Beatric Askul Moe ameapishwa kuwa Waziri mpya wa Masuala ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Maendeleo ya Kikanda na Ustawi wa Maeneo Kame (ASAL).

Bi Askul pia ameweka historia kama mwanamke wa kwanza kutoka jamii ya Waturkana kuwahi kuhudumu kama Waziri katika serikali ya kitaifa tangu taifa hili lilipopata uhuru 1963.

Wawili hao waliapishwa katika hafla fupi iliyoshuhudiwa na Rais William Ruto katika Ikulu ya Nairobi.

Wengine waliohudhuria shughuli hiyo ni Naibu Rais Rigathi Gachagua, Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi, mawaziri, wabunge wanaoshikilia nyadhifa za uongozi katika bunge la kitaifa.

Teuzi za Bi Oduor na Bi Askul na Rais Ruto ziliidhinishwa na wabunge Jumatano, Agosti 14, 2024 kwa kupitisha ripoti ya Kamati ya Uteuzi iliyowapiga msasa kubaini ufaafu wao wa vyeo hivyo mnamo Agosti 9, 2024.

“Ni rasmi sasa bunge hili limeidhinisha uteuzi wa Bi Dorcas Agik Odhong Oduor kuwa Mwanasheria Mkuu na Bi Beatrice Askul Moe kuwa Waziri wa Masuala ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Maendeleo ya Kikanda na Ustawi wa Maeneo Kame,” akasema Bw Wetang’ula baada ya wabunge kupiga kura ya NDIO kwa ripoti hiyo.

“Ni rasmi sasa bunge hili limeidhinisha uteuzi wa Bi Dorcas Agik Odhong Oduor kuwa Mwanasheria Mkuu na Bi Beatrice Askul Moe kuwa Waziri wa Masuala ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Maendeleo ya Kikanda na Ustawi wa Maeneo Kame,” akasema Bw Wetang’ula baada ya wabunge kupiga kura ya NDIO kwa ripoti hiyo.

Akiongea Jumanne baada ya wawili hao kuapishwa, Rais Ruto aliwahakikishia kuwa atawaunga mkono wanapotekeleza majukumu yao.

Alimtaka Bi Oduor kuhakikisha kuwa afisi yake inatekeleza ipasavyo wajibu wake wa kutoa ushauri wa kisheria kwa serikali kuu na asasi zake zote.

“Afisi ya Mwanasheria Mkuu inafaa kushirikiana na wizara za serikali na asasi nyinginezo kuhakikisha kuwa serikali inapata ushauri na uwakilishi sawa. Hakikisha kwamba afisi yako inalinda masilahi ya umma nyakati zote,” Rais Ruto akasema.

Kiongozi wa taifa pia alimhimiza Bi Askul kama Waziri wa Masuala ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kuhakikisha kuwa Kenya inapata uwakilishi sawa katika jumuiya hiyo.