Habari za Kitaifa

Jinsi mshukiwa wa mauaji ya Kware alivyosaidiwa kutoroka seli za polisi


MASWALI yameibuka baada ya mshukiwa mkuu wa mauaji ya wanawake 42, ambao miili yao ilipatikana imetupwa kwenye timbo mtaani Kware, Embakasi, kutoroka katika Kituo cha Polisi cha Gigiri, Nairobi.

Collins Jumaisi Khalusha, ambaye ilidaiwa alikiri kuhusika na mauaji hayo ambayo baadaye yalipunguzwa kuwa ya wanawake sita, alikuwa miongoni mwa washukiwa 13 waliotoroka kutoka seli za kituo hicho cha polisi, saa tisa alfajiri Jumanne.

Kaimu Inspekta Jenerali wa polisi, Gilbert Masengeli alisema maafisa wanane waliokuwa kazini walisimamishwa kazi na kukamatwa kwa kusaidia mahabusu hao kutoroka.

Maafisa ambao walikamatwa mara moja ni pamoja na Kamanda wa polisi wa Kaunti ndogo ya Gigiri, afisa mkuu wa kituo hicho na wengine sita miongoni mwao waliokuwa katika afisi ya kupokea ripoti na mlinzi wa seli.

Bw Masengeli alisema maafisa hao walilengwa baada ya uchunguzi wa awali kuonyesha kutoroka kwa mahubusu hao kulikuwa “kazi ya ndani” ya maafisa waliokuwa zamu na wengine.

“Tunachunguza tukio hilo na uchunguzi wetu wa awali unaonyesha kuwa, walisaidiwa kutoroka na watu wa ndani ya kituo, ikizingatiwa kuwa maafisa walikuwa wamewekwa ipasavyo kulinda kituo,” Bw Masengeli alisema.

“Kwa hivyo, nimewasimamisha kazi maafisa wanane waliokuwa zamu jana usiku.” Kituo hicho kiko katika eneo la kimkakati ambayo inafanya vigumu kwa mahabusu kutoroka.

Kutoroka kwa Jumaisi kunaibua maswali hasa ikizingatiwa kuwa alihepa siku chache kabla ya kurudishwa kortini alikotarajiwa kufunguliwa mashtaka ya mauaji.Polisi walitarajiwa kumfikisha kortini Ijumaa Agosti 23 baada ya kukamilisha uchunguzi.

Vile vile, kutoroka kwake na washukiwa wengine kumeibua maswali hasa ikizingatiwa ulinzi mkali unaopaswa kupatiwa washukiwa wa mauaji na siku chache kabla ya kufunguliwa mashtaka. Bw Masengeli alisema kulikuwa na mahabusu 17 katika seli na ni wanne waliobaki.

Alisema kwamba, waliotoroka pamoja na Jumaisi ni raia wa Eritrea 12 waliozuiliwa katika kituo hicho kwa kuwa nchini kinyume cha sheria.

Kamanda wa polisi Nairobi Adamson Bungei ambaye awali alithibitisha kisa hicho, alisema msako umeanzishwa ili kuwakamata tena mahabusu waliotoroka.

“Tunafuatilia suala hilo kwa lengo la kuchukua hatua,” alisema.

Ripoti ya polisi iliyonakiliwa katika kituo hicho, OB 05/20/08/2024, ilionyesha kuwa kisa hicho kiliripotiwa na maafisa wa polisi Evans Kipkirui na Gerald Mutuku waliokuwa wakisimamia seli hizo.

Maafisa hao walisema walifanya ziara yao ya kawaida katika seli wakiwa na meneja wa hoteli ya polisi ili kuwapa mahabusu kiamsha kinywa walipogundua washukiwa walikuwa wametoroka.

Walisema walipofungua mlango wa seli, walishtuka baada ya kubaini kuwa watuhumiwa 13 walikuwa wametoroka kwa kukata waya kwenye eneo la kuotea jua.

Jumaisi alikuwa seli, akisubiri kufikishwa mahakamani Ijumaa, Agosti 23, 2024.

Ingawa polisi walisema alikuwa amekiri kuua wanawake 42 na kutupa miili yao katika timbo huko Kware, walidai wangemshtaki kwa mauaji ya wanawake sita pekee ambayo walikuwa wamethibitisha.

Kwa mujibu wa duru zilizozungumza na Taifa Leo, Jumaisi, 33, ambaye awali polisi walisema alikiri kuwaua wanawake 42 akiwemo mkewe alipata kifungua kinywa katika kituo cha polisi.

Kiamsha kinywa katika seli za polisi kwa kawaida hutolewa baada ya mahabusu kuhesabiwa kunakofanyika kati ya saa kumi na moja na saa kumi na mbili alfajiri.

Hii inamaanisha kuwa, mfungwa huyo alikuwa ndani ya seli baada ya 12 kutoweka. Kutokana na maelezo haya, maswali ya kutatanisha ni: Jumaisi alitoroka saa ngapi? Na katika hali gani?

Duru ziliiambia Taifa Leo kwamba, Jumaisi alisaidiwa kutoroka baada ya wengine kwa sababu ya mzozo kuhusu mpango wa kusaidia mahabusu wengine kuhepa.

Taifa Leo ilibaini kuhusu madai ya ugomvi kati ya maafisa fisadi kuhusu pesa ambazo Waeritrea walidaiwa kulipa ili kununua uhuru wao.

Kulingana na mdokezi wetu, wale waliohisi kutengwa walipopata Waeritrea 12 hawakuwepo, walichagua kupaka matope wenzao kwa kumwachilia Jumaisi ambaye angevutia hasira kali zaidi za umma.