Habari za Kitaifa

Naibu kuchukua usukani baada ya Mwangaza kuzimwa

Na DAVID MUCHUI August 21st, 2024 1 min read

BAADA ya kufungiwa nje ya mikutano ya baraza kwa zaidi ya mwaka mmoja, Naibu Gavana wa Kaunti ya Meru, Isaac Mutuma M’Ethingia, anatazamiwa kuchukua usukani wa kaunti hiyo kama gavana.

Hii ni baada ya Seneti Jumanne usiku, Agosti 20, 2024 kupitisha uamuzi wa kumtimua Gavana Kawira Mwangaza na kufikisha kikomo utawala wake wa miaka miwili Meru.

Hata hivyo, Bi Mwangaza alipata agizo la kusimamisha kutimuliwa kwake na seneti.

Gavana Mwangaza na na naibu wake, Mutuma waliapishwa pamoja rasmi Agosti 25, 2022.

Kifungu 182 cha Katiba kinasema gavana anapong’atuliwa mamlakani, naibu wake huchukua usukani kwa muda uliosalia.

Bw Mutuma, 44, ni kasisi aliyetawazwa na Kanisa la Methodist na alijitosa katika siasa kwa mara ya kwanza 2022 wakati Bi Mwangaza alimteua kuwa mgombea mwenza wake.

Aliwahi kufanya kazi kama afisa wa magereza na ni mwanawe aliyekuwa mwenyekiti wa baraza la wazee wa jamii ya Ameru, Njuri Ncheke, marehemu Paul M’Ethingia.

Bw Mutuma ana shahada ya digrii katika Theolojia kutoka Chuo Kikuu cha Kenya Methodist (KeMU).

Siku chache kabla ya Uchaguzi Mkuu Agosti 2022 kufanyika, Gavana Mwangaza alisema alimteua Bw Mutuma kama mgombea mwenza wake ‘baada ya maombi na majadiliano ya kina.

“Nililelewa katika familia maskini na nikasomea Shule ya Msingi ya Maua. Baada ya sekondari, nilijiunga na Huduma ya Magereza Nchini 2002 na kuhudumu kwa miaka 19. Niliondoka kama sajini mkuu na afisa wa maslahi katika magereza,” alisema Pasta Mutuma katika mahojiano.

Anahoji kuwa wadhifa aliohudumu kama kiongozi katika Kanisa la Methodist, ulimwezesha kupata ufadhili wa elimu kusomea Theolojia, KeMU na kufuzu 2019. “Nilipokuwa nikihudumu kama mtumishi wa Methodist, Gavana Mwangaza aliniona. Aliwasiliana nami Desemba 2020 na tukaafikiana kuwa naweza kuwa mgombea mwenza wake,” alisema.

“Gavana ni askofu na mimi ni mchungaji hivyo tunaleta uongozi unaofaa Meru. Tuna maadili mema kumaanisha vitendo vya ufisadi haviwezi kufanyika Meru. Jinsi Biblia inavyosema, watakatifu wanapotawala, watu hushangilia,” alisema katika mahojiano.