Makala

Mwimbaji wa Zabron Singers kutoka Tanzania afariki


MWIMBAJI Marco Joseph wa kundi la waimbaji la Zabron kutoka Tanzania, linakojulikana kwa nyimbo zao maarufu za Kiswahili, ukiwemo uliovuma katika kampeni ya Rais William Ruto 2022, amefariki.

Alifariki dunia Agosti 21, 2024, kutokana na ugonjwa wa moyo alipokuwa akipatiwa matibabu katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Katika mahojiano kwa simu na ‘Taifa Leo Dijitali,’ dadake Marco, Victoria Zabron, alisema kakake alianza kuugua wiki moja iliyopita siku chache kabla ya tamasha waliloshiriki Kisumu.

“Alilazimika kubaki nyuma kutafuta matibabu, madaktari walisema moyo wake ulikuwa na tatizo lililohitaji kufanyiwa upasuaji wa dharura, alikuwa akipatiwa matibabu ya moyo katika Hospitali ya Muhimbili lakini haukufaulu, mazishi yatafanyika Mikocheni, nyumbani kwa shangazi yake. Kwa sasa, mwili bado uko katika mochari,” Victoria alisema.
Kulingana na Mwenyekiti wa Kwaya ya Zabron Singers, Japeh Zabron, kaka yake alipatwa na mshtuko wa moyo walipokuwa ziarani Kenya siku chache zilizopita.

Juhudi za kumtibu zilifanyika katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando, lakini alipewa rufaa ya kwenda JKCI kwa matibabu zaidi kabla ya kufariki dunia akipatiwa matibabu.
Miongoni mwa nyimbo alizotamba nazo akiwa na kundi hilo ni pamoja na “Mkono wake Bwana,” “Swetie Sweetie,” “Sisi Ndio Wale,” “Uko Single,” “Nakutuma Wimbo,” na nyingine nyingi.
Kakake mdogo, Japhet Zabron, pia amemsifu mwimbaji huyo.

“Sikutaka kupost chochote kuhusu hili maana nilikuachia wewe Mungu lakini Mungu sasa umenifanyia hiki hiki. Nooooo hawezi kuwa hivi hapana🙌🏽 Ooh God no.” aliandika kwenye mitandao ya kijamii Waimbaji wa Zabron walipata umaarufu kupitia wimbo wao wa ‘Mkono Wa Bwana.’
Tangu wakati huo, wamewavutia mashabiki kwa nyimbo nyingine nyingi.

Wanachama wengine wa kwaya hiyo ni pamoja na Victoria Zabron, Jamila Dotto, Samuel Joseph, Semroza Godfrey, Grace Madata na Joyce Zabron.
Katika mahojiano yaliyopita, Japhet, mwalimu wa kikundi alikumbuka jinsi kikundi kiliibuka:

“Tulipokuwa tukisoma sekondari tulienda studio tukarekodi wimbo, hatukuwa na pesa ikabidi tukope kwa watu ili kulipia muda wa studio, ulirekodiwa vibaya hata tukaona aibu kuutoa wimbo huo. Karibu tukate tamaa.”

Wimbo wa “Mkono wa Bwana” ulivuma wakati wa kampeni za Rais William Ruto na kupelekea Zabron Singers kutunukiwa heshima ya kutumbuiza katika hafla ya kuapishwa kwake.