HabariHabari za Kitaifa

Uteuzi wa Joho kama waziri wapingwa Mahakama Kuu

Na CAROLINE WANJUGU August 23rd, 2024 Kusoma ni dakika: 2

UAMUZI wa Rais William Ruto kumteua Hassan Joho katika Baraza la Mawaziri umepingwa katika Mahakama Kuu walalamishi wakitaka gavana huyo wa zamani wa Mombasa ang’olewe afisini.

Katika kesi iliyowasilishwa Mahakama Kuu ya Nairobi na kuidhinishwa kuwa ya dharura, shirika la Genesis for Human Rights Commission linahoji kuwa uteuzi wa Bw Joho kama Waziri wa Madini na Uchumi wa Baharini ulikiuka katiba kwa misingi ya kiwango cha elimu kinachohitajika.

Aidha, shirika hilo pia limejumuisha Bunge la Kitaifa, Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) na Tume ya Kusimamia Elimu ya Vyuo Vikuu katika kesi hiyo.

Shirika linadai kuwa taasisi hizo tatu zilikosa kuzingatia nakala ilizowasilisha ambazo zina ushahidi kwamba Bw Joho hafai kwa uteuzi, likisema hajatimiza masharti ya kufuzu kielimu kama inayohitajika kwa mtu kuteuliwa kama waziri.

Linahoji kuwa Bunge na EACC zilikosea kumwidhinisha Bw Joho ateuliwe.

Genesis for Human Rights pia linahoji kwamba wakati wa uteuzi wake Bw Joho alikuwa mmoja wa manaibu wa kinara wa Orange Democratic Movement (ODM), chama cha walio wachache bungeni na hivyo kama upinzani alikuwa na jukumu la kupiga darubini utendakazi wa serikali.

Bw Joho baada ya kuchukua hatamu kama Waziri wa Madini  akiwa katika ofisi hiyo kwenye jumba la Works Building, Nairobi, mapema Agosti 2024. PICHA | MAKTABA

Katika stakabadhi zilizowasilishwa kortini, mlalamishi anataka Mahakama Kuu itangaze kuwa uteuzi wa Bw Joho kama Waziri wa Madini ni kinyume cha katiba, ufutiliwe mbali, na mtu mwingine anayefaa apigwa msasa ili kuteuliwa katika wadhifa huo.

Kupitia hati ya kiapo kortini Bw Caleb Ngwena – ambaye ni mkazi wa Bamburi katika Kaunti ya Mombasa – anasema Bw Joho hafai kushikilia afisi hiyo kwa sababu amehusishwa na madai ya uhalifu wa kiuchumi na ulanguzi wa mihadarati, kulingana na ripoti iliyowasilishwa bungeni na marehemu Profesa George Saitoti, ikiwemo kufuja fedha za umma alipohudumu kama Gavana wa Mombasa.

Akipokea nakala hiyo ya kiapo, Jaji Lawrence Mugambi aliamuru hati za kesi hiyo ziwasilishwe kwa mshtakiwa katika kipindi cha siku saba.

Kesi hiyo itatajwa Oktoba 17, 2024.

Bw Joho alichukua usukani kama Waziri wa Madini kutoka kwa Bw Salim Mvurya, ambaye sasa ni Waziri wa Uwekezaji, Biashara na Viwanda. Hii ni baada ya Rais William Ruto kuapisha Baraza jipya la Mawaziri mapema Agosti 2024.