Habari za Kitaifa

Kenya yathibitisha kisa cha pili cha Mpox

Na LEON LIDIGU, WINNIE ONYANDO August 23rd, 2024 Kusoma ni dakika: 1

KENYA imethibitisha kisa cha pili cha virusi vya Mpox.

Kisa hicho kimethibitishwa na Katibu Katika Wizara ya Afya Mary Muthoni na mwenzake wa Idara ya Masuala ya Dawa kwenye Wizara ya Afya Harry Kimtai.

Hii ni baada ya dereva wa lori kutoka Uganda kupatikana na Mpox eneo la Malaba.

Dereva huyo aligunduliwa na virusi hivyo alipopimwa katika eneo la Malaba One Stop Boarder Post-Kaunti ya Busia.

“Dereva huyo ametengwa na yuko chini ya uangalizi katika mojawapo ya vituo vyetu vya afya katika Kaunti ya Busia. Zaidi ya hayo, uchunguzi wa kina wa visa vinavyoshukiwa umeimarishwa katika eneo hili na katika kaunti zote ili kuhakikisha ugonjwa huo unadhibitiwa,” Waziri huyo alisema katika taarifa kwa vyombo vya habari Ijumaa.

Dkt Barasa alisema hadi sasa jumla ya sampuli 42 zimewasilishwa kwenye maabara ili kupimwa na tayari sampuli 40 zimethibitishwa kuwa hazina ugonjwa huo.

“Aidha, tumewapima jumla ya wasafiri 426,438 katika Bandari zetu mbalimbali za Kuingia nchini kote,” aliongeza.

Afisa mkuu katika wizara hiyo ambaye hana mamlaka ya kuzungumza na vyombo vya habari, alisema kwa sasa wamechanganyikiwa kuhusu nani anafaa kutoa taarifa rasmi kwa vyombo vya habari.

“Kisa hicho kiligunduliwa Alhamisi Agosti 23, 2024 lakini kwa sababu ya mvutano kati ya Katibu Muthoni na Dkt Amoth, tumelazimika kusubiri hadi wazungumze na kukubaliana ni nani tunafaa kumpa taarifa hizo,” akasema afisa huyo.

Maambukizi ya Mpox kutoka mtu mmoja hadi kwa mwingine yanaweza kusambaa kwa kugusana moja kwa moja na ngozi ya mtu aliyeambukizwa au vidonda vingine, kama vile mdomoni au kwenye sehemu za siri.