Fahamu jinsi mzazi anaweza kumuandikisha mwanafunzi katika bima ya SHIF
WIZARA ya Elimu imetoa wito kwa wazazi wenye wanafunzi katika shule za msingi na upili kuwasajili kwa Hazina ya Bima ya Kijamii (SHIF) kabla ya shule kufunguliwa Jumatatu, Agosti 26, 2024.
Kwenye taarifa, Katibu wa Wizara ya Elimu Belio Kipsang’ aliagiza kuwa wanafunzi hao wasajiliwe kuwa wategemeaji wa wazazi wao.
Hazina ya SHIF inatarajiwa kuchukua mahala pa Hazina ya Kitaifa ya Bima ya Afya (NHIF) kuanzia Oktoba 1, mwaka huu.
“Usajili wa Wakenya kwa Hazina ya Afya ya Jamii ulianza Julai 1, 2024 kama njia ya kuwezesha kufikiwa kwa Mpango wa Afya kwa Wote. Kwa hivyo wanafunzi wote wanahitajika kusajiliwa kama wategemeaji wa wazazi wao kabla ya tarehe ya shule kufunguliwa kwa muhula wa tatu wa mwaka wa masomo wa 2024,” Dkt Kipsang’ akasema.
Katibu huyo alisema kuwa usajili huo unaweza kufanywa kwenye majukwaa ya mitandaoni kupitia tovuti ya www.sha.go.ke au www.afyangua.go.ke au kwa njia ya simu kupitia nambari *147#.
Dkt Kipsanga alisema kuwa endapo wazazi watakumbwa na changamoto zozote wakati wa usajili huo, wanafaa kuwasiliana na Mamlaka ya Afya ya Kijamii kupitia nambari ya simu 0800720601 au watume barua pepe kwa anwani [email protected].
Agizo la wizara ya elimu kuhusu usajili kwa bima ya SHIF limetoa afueni kwa wazazi na wanafunzi waliopoteza bima yao ya afya baada ya serikali kutatisha Mpango wa Bima wa EduAya.
Bima hiyo iliyogharimu Sh4.5 bilioni ilinufaisha zaidi ya wanafunzi 3.4 milioni katika shule za msingi na upili.
Hii ndio maana kutamatishwa kwa mpango huo mwishoni mwa Desemba 31, 2023 kuliibua malalamishi kutoka kwa wazazi, walimu wakuu na wanafunzi wenyewe.
Sheria ya Bima ya SHIF ilitiwa saini na Rais William Ruto mnamo Machi 23, 2023 lakini haijaanza kazi kufuatia kesi zilizowasilishwa kortini kupinga uhalali wake.
Kwa mujibu wa sheria hiyo, familia masikini kabisa zinapasa kuchangia Sh300 kila mwezi kwa bima ya SHIF.
Kwa upande mwingine watu ambao wameajiriwa na hupokea mishahara kila mwezi wanapaswa kuchanga asilimia 2.75 ya mishahara hiyo.