Habari za Kitaifa

Karoney, Tunai warushiwa minofu, Nyakera akihamishwa KEMSA

Na LABAAN SHABAAN August 24th, 2024 1 min read

RAIS William Ruto amemteua aliyekuwa Gavana wa Narok Samuel Tunai kuwa Mwenyekiti wa Mamlaka ya Usambazaji wa Bidhaa za Matibabu nchini (KEMSA).

Bw Tunai atachukua nafasi ya aliyekuwa Katibu katika Wizara ya Uchukuzi Irungu Nyakera baada ya uteuzi wake kubatilishwa.

Bw Nyakera aliteuliwa mwenyekiti wa bodi mpya ya KEMSA mwaka wa 2023.

Hii ni baada ya Rais kuwasimamisha kazi kwa muda wanachama wa bodi ya KEMSA kuhusiana na sakata ya usambazaji wa neti za mbu ya Sh4 bilioni.

Awali Bw Tubai aliteuliwa kuwa Waziri Msaidizi (CAS) katika Wizara ya Usalama wa Ndani kabla ya korti kuamua kuwa nafasi hizo ni kinyume cha sheria.

Wakati uo huo, Bw Nyakera ameteuliwa kuwa mwenyekiti wa bodi ya Jumba la Mikutano ya Kimataifa la KICC.

Atachukua nafasi ya aliyekuwa Naibu Gavana wa Makueni Adeline Mwau aliyeteuliwa katika wadhifa huo Aprili 2023.

“Nikifuata mamlaka niliyopewa na sehemu ya 5(1) ya Sheria ya KEMSA, ikisomwa pamoja na sehemu ya 51(1) ya Sheria ya Ufafanuzi na Maelekezo ya Jumla kuhusu Mikataba, mimi, William Samoei Ruto, Rais wa Jamhuri ya Kenya na Amiri Jeshi Mkuu wa Ulinzi, ninamteua Samuel Tunai kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa KEMSA, kwa muda wa miaka mitatu (3) kuanzia Agosti 23, 2024,” ilieleza sehemu ya gazeti rasmi la serikali.

Kiongozi wa Taifa pia alimteua aliyekuwa Waziri wa Ardhi Farida Karoney kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Kitaifa ya Kamari kwa kipindi cha miaka mitatu.

Naye Prof Jeremiah Nyabuti ameteuliwa kuwa mwanachama wa Bodi ya Usajili wa Mipango ya Ustawishaji wa Ardhi kwa miaka mitatu.