Habari za Kitaifa

Tahadhari: Ukila nyama ya pori unaweza kupata Mpox


WAZIRI wa Utalii na Wanyamapori, Rebecca Miano, ametoa wito kwa Wakenya kuepuka kushika au kula nyama ya wanyamapori kutokana na tishio la ugonjwa wa Mpox. 

Bi Miano alisema kuwa japo waliopatikana na ugonja huo wametengwa, huenda ugonjwa huo ukaenea ikiwa Wakenya watakosa kutii ushauri wa tahadhari kutoka kwa wataalamu.

Wataalamu wa matibabu na afya ya wanyama wanasema Mpox ni ugonjwa wa virusi vya zoonotic kwa maana kuwa unaweza kuambukizwa kati ya wanyama pori na wanadamu.

Kulingana na wataalamu kuenea kwa maradhi ya zoonotic-iwe ya bakteria, virusi au vimelea-hutokea kwa njia ya kutangamana moja kwa moja au kula chakula sawa au kunywa maji sawa.

Kulingana na Bi Miano ugonjwa huo huenea haraka pale ambapo watu wanapotangamana na wanyama pori.

“Katika siku hii na enzi hii ya matokeo mabaya ya mabadiliko ya hali ya hewa, mienendo ya viini vinavyosambazwa na wadudu (vector pathogen) inaweza kusababisha kuibuka kwa magonjwa ambayo hayajawahi kushuhudiwa. Niliwahimiza Wakenya kujiepusha na nyama ya wanyama wa porini,” alisema waziri.

Shirika la Huduma ya Wanyamapori nchini (KWS) na Taasisi ya Utafiti na Mafunzo ya Wanyamapori (WRTI) zinashirikiana kwa karibu na Kurugenzi ya Huduma ya Mifugo na Wizara ya Afya kukomesha milipuko zaidi ya Mpox katika eneo hilo.

Bi Miano alisema madaktari wa mifugo katika mashirika haya ya serikali wanafuatilia kwa karibu hali ya afya ya watu na wanyamapori.

“Tuko katika hali ya tahadhari kufuatia ripoti za mlipuko wa hivi karibuni wa Mpox katika eneo hilo. KWS na WRTI ni sehemu ya timu ya kitaifa ya usimamizi wa Mpox kwa sasa inayopokea taarifa kuhusu milipuko hiyo,” alisema CS katika taarifa.

Maagizo yake yanajiri siku moja tu baada ya serikali kuthibitisha kisa cha pili cha ugonjwa huu Kenya.

Mgonjwa wa pili aliyethibitishwa ni dereva wa lori kutoka Uganda.

Dereva huyo aligunduliwa na virusi hivyo alipopimwa katika eneo la Malaba One Stop Boarder Post-Kaunti ya Busia.

‘Dereva huyo ametengwa na yuko chini ya uangalizi katika mojawapo ya vituo vyetu vya afya katika Kaunti ya Busia. Zaidi ya hayo, uchunguzi wa kina wa visa vinavyoshukiwa umeimarishwa katika eneo hili na katika kaunti zote ili kuhakikisha ugonjwa huo unadhibitiwa,’ Waziri huyo alisema katika taarifa kwa vyombo vya habari jana.

Dkt Barasa alisema hadi sasa jumla ya sampuli 42 zimewasilishwa kwenye maabara ili kupimwa na tayari sampuli 40 zimethibitishwa kuwa hazina ugonjwa huo.

‘Aidha, tumewapima jumla ya wasafiri 426,438 katika Bandari zetu mbalimbali za Kuingia nchini kote,’ aliongeza.