Habari za Kaunti

Makao mapya ya Kisii kugharimu mlipa ushuru Sh500 milioni

Na WYCLIFFE NYABERI August 29th, 2024 1 min read

SERIKALI ya Kaunti ya Kisii imezindua ujenzi wa makao yake mapya, yatakayogharimu mlipa ushuru kima cha Sh500 milioni.

Ujenzi wa makao hayo mapya, utachukua muda wa miaka miwili na utatekelezwa na kampuni ya Uchina ya Fubeco (China Fushun)

Akiongea wakati wa kuweka jiwe la msingi la mradi huo mpya, Gavana wa Kisii Simba Arati alisema makao hayo yatakapokamilika, yatakuwa na sehemu maalum kama vile pahala pa kina mama kunyonyeshea watoto.

“Tutajenga afisi za kisasa na za kupendeza. Huduma zote za serikali ya Kisii zitakuwa chini ya paa moja,” Gavana Arati alisema.

Mbunge huyo wa zamani wa Dagoretti Kaskazini aliongeza kuwa wafanyakazi wengi wa serikali ya Kisii wamekuwa wakihangaika kutekeleza majukumu yao kwa kuwa hawana afisi maalum.

Bw Arati aidha alisema, afisi za sasa za wafanyakazi wa kaunti, ziko katika sehemu mbalimbali za mji wa Kisii na hivyo walikuwa wakitumia rasilimali nyingi kuzimudu.

“Ujenzi huu utakapokamilika, utawafaa wafanyakazi wengine wa kaunti, ambao hawana afisi kupata mahali pa kufanyia kazi. Pia, tutaweza kuchukua data za wafanyakazi wanaoripoti kazini na wale wanaokosa kimakusudi kwa urahisi,” Gavana Arati alisema.

Gavana wa kwanza wa Kaunti ya Kisii, Bw James Ongwae, alipoingia afisini 2013, aliweka afisi zake katika majengo ya zamani yaliyokuwa yanatumiwa na Manispaa ya Mji wa Kisii.

Lakini baada ya kumrithi mwaka 2022, Gavana Arati hakuwahi kuingia katika afisi zilizokuwa zinatumiwa na mtangulizi wake.

Aliamua kutumia afisi za wageni mashuhuri zilizoko katika uwanja wa michezo wa Gusii.

Afisi hizo ziliimarishwa viwango baada ya uga huo kuandaa sherehe za Mashujaa Dei mwaka 2020.

Bw Arati, pia, aliweka kiasi fulani cha pesa kufanyia ukarabati zilizokuwa afisi za Bw Ongwae na ujenzi huo ungali unaendelea.