Gavana wa zamani asubiri zaidi ya saa 5 korti imhukumu kwenye kesi ya ufisadi
GAVANA wa zamani Samburu, Bw Moses Lenolkulal Alhamisi, Agosti 29, 2024 alilazimika kusubiri kwa zaidi ya saa tano korti kumhukumu kufuatia kesi inayomuandama ya ufisadi.
Huku Lenolkulal akisubiri kujua hatma yake, Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Rensong Ingonga aliitaka mahakama ya kukabiliana na ufisadi kutoa adhabu kali kwa gavana huyo wa kwanza Samburu.
Hii ni baada ya kupatikana na hatia ya ufisadi, ambapo alitumia kampuni yake ya mafuta ya Oryx Services kufuja pesa za umma.
DPP kupitia mawakili Riungu Gitonga, Alex Akula, Wesley Nyamache na Delroy Mwasaru walimweleza hakimu mkuu Thomas Nzioki atoe adhabu hiyo kwa sababu ya kukiuka imani kwa watu wa Samburu ambao mahakama hiyo ilitaja kuwa wametengwa.
Riungu aliwasilisha kwamba gavana huyo wa zamani alipokea kwa njia ya ufisadi zaidi ya Sh83 milioni kutoka kwa pesa zilizotengewa kaunti kutoka kwa hazina ya kitaifa kwa kufanya biashara ya kibinafsi na taasisi aliyokuwa akiongoza.
“Ufisadi unapaswa kufanywa mchungu na mahakama hii inaweza kutoa agizo la kutwaa mali iliyopatikana kupitia pesa zilizopokelewa kwa ufisadi kutoka kwa kaunti,” Riungu alisema.
Hakimu wa mahakama aliambiwa kuwa Lenolkulal alimleta mfanyabiashara Hesbon Ndathi ili kufunika matendo yake.
“Oryx Services Limited ilikuwa chombo cha uhalifu kwa kuwa Sh83, 335, 255 zililipwa kutoka kwa serikali ya Kaunti ya Samburu. Gavana Lenolkulal hakujiendesha kwa njia ya uwazi,” Riungu alisema huku akiitaka mahakama kutimiza adhabu stahiki kama ilivyoainishwa chini ya miongozo ya hukumu.
Maamuzi ya hukumu ya Bw Lenolkulal yalisubiriwa kwa zaidi ya saa matano.
Hadi wakati wa kuchapisha taarifa hii, korti haikuwa imetoa hukumu dhidi yake.
Imetafsiriwa na Wycliffe Nyaberi