Aliyetemwa na mzungu arejea kuchonga mawe
Na SAMUEL BAYA
Kanamai, Kilifi
KALAMENI aliyebeza wanakijiji baada ya kufanikiwa kupata demu mzungu sasa anajuta baada ya demu huyo kuamua kumkimbia.
Jamaa huyo sasa amelazimika kurudi mitaani na kuchangamkia vibarua kujipatia riziki.
Kwa mujibu wa mdokezi, jamaa alikuwa mmoja wa waliokuwa wakizungusha watalii katika ufuo wa Kikambala miaka kadhaa iliyopita alipofanikiwa kumpata kidosho kutoka UfaranSa ambaye aliamua kumuoa.
Hata hivyo, ndoa yao ilibakia tu ya kuishi hoteli moja baada ya nyingine huku mara nyingi demu akiwa kwao Paris.
Mzungu huyo kulingana na majirani aligeuza kwa haraka maisha ya jamaa ambaye baada ya muda alikuwa akiendesha magari ya kifahari.
“Huyu jamaa aliitupa bahati,” alisema jirani mmoja ambaye alihadithia yaliyomsibu kijana huyo hadi akafilisika na sasa anasota mitaani.
“Huyu jamaa alibadilika na kuanza kuishi maisha ya hali ya juu. Hata wazazi wake ambao ni maskwota alishindwa kuwajengea nyumba,” alisema mdokezi
Yasemekana jamaa aliponda raha katika hoteli za kifahari katika mji wa Mtwapa na kusahau kabisa nyumbani.
“Kwao ni hapa tu lakini alikuwa akionekana Mtwapa, Diani na Ukunda. Hakumshauri mzungu huyo kwamba hata wazazi wake walihitaji mahali pa kuishi,” alisema mdokezi wetu.
Hata hivyo mwaka jana, mambo yalienda kombo alipokosana na mzungu huyo ambaye aliamua kuondoka na kurudi kwao.
Inadaiwa kwamba jamaa alianza kumtandika kipusa kila alipokuwa amelewa, jambo ambalo lilimkera mzungu huyo.
Jombi alirudi kijijini baada ya kumaliza fedha alizokuwa amebakisha .
“Amerudi kijijini akiwa na aibu. “Kwa sasa jamaa amekubali hali yake na huwa anaenda timboni kuchonga mawe,” aliongeza mdokezi wetu.