Habari

DPP apewa siku 15 kumpa Devani ushahidi

Na RICHARD MUNGUTI August 30th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

MKURUGENZI wa Mashtaka ya Umma (DPP) Renson Ingonga amepewa siku 15 na mahakama ya kuamua kesi za ufisadi (ACC) kutoa ushihidi dhidi ya bwanyenye Yagnesh Devani katika kesi inayomkabili ya kashfa ya mafuta ya ndege ya Sh7.6 bilioni.

Kupitia kwa kiongozi wa mashtaka Jeremiah Walusala, DPP alieleza hakimu mkuu mnamo Ijumaa Agosti 30,2024 kwamba, ushahidi anaotazamia kumkabidhi  Devani uko mbele ya hakimu mwandamizi Robinson Ondieki.

Walusala alisema Ondieki anaendelea kusikiza kesi nyingine  dhidi ya Devani ya ulaghai wa Sh1.5 bilioni.

Mahakama ilielezwa ushahidi huo huo ndio utakaowasilishwa katika kesi hii ya ufisadi inayomkabili Devani.

Mawakili Mwenda Mbaka na Moses Kurgat wanaomwakilisha Devani hawakupinga ombi hilo.

Hakimu Nzioki alikubalia ombi hilo na kuagiza kesi hiyo itajwe Septemba 16,2024 na DPP aeleze mahakama ikiwa alimkabidhi mshtakiwa nakala za mashahidi.

Alitoroka Kenya

Devani alikamatwa na kurudishwa nchini Januari 2024 kutoka Uingereza alikotorokea miaka  15 iliyopita.

Alikuwa amewasilisha kesi katika mahakama ya Uingereza kupinga kurudishwa nchini lakini kesi hiyo ikatupiliwa mbali.

Serikali ya Kenya ilikuwa imepata kibali cha kumtia nguvuni Devani.

Polisi wa humu nchini wakishirikiana na polisi wa kimataifa (Interpol) walifaulu kumkamata Devani.

Aliporejeshwa nchini, Devani alifunguliwa kesi mbili.

Akipinga kurudishwa Kenya, Devani alidai “magereza ya Kenya ni machafu kupindukia.”

Pia alieleza mahakama Uingereza kwamba “hatapata haki katika mahakama za Kenya endapo atarudishwa kufunguliwa mashtaka ya ulaghai wa lita 126,000,000 za mafuta ya ndege ya thamani ya Sh7.6 bilioni.”

Devani alikanusha mashtaka 11 aliyoshtakiwa na mkurugenzi wa mashtaka ya umma (DPP) ya ulaghai wa mafuta ya ndege lita 19,186,130 ambayo kampuni yake Triton Petroleum Company iliilaghai kampuni ya ng’ambo ya Emirates National Oil Company iliyoko nchini Singapore.

Bw Nzioki alipokea ripoti ya idara ya urekebishaji tabia iliyomhoji Devani kubaini masuala kadhaa kuhusu tabia yake tangu arudishwe nchini Januari 23,2024.

Ripoti hiyo iliyoruhusu Devani aachiliwe kwa dhamana ilisema, “Tabia yake sio mbovu na kwamba ameoa na yuko na familia nchini Kenya.”

Pia hakimu alielezwa Devani amewekeza mabilioni ya pesa nchini.

Devani aliachiliwa kwa dhamana na kuonywa asiwavuruge mashahidi.