Habari za Kitaifa

Wakuu wa vyuo wapongeza mfumo tata wa ufadhili

Na WINNIE ATIENO August 31st, 2024 2 min read

MANAIBU Chansela kutoka vyuo vikuu vya umma na vya kibinafsi wameunga mkono mfumo mpya wa ufadhili ambao umegeuka kitendawili kigumu kwa serikali ya Kenya Kwanza ya Rais William Ruto.

Haya yanajiri huku kukiwa na shinikizo kali kutoka kwa wadau wakiwemo wanafunzi wa vyuo vikuu wanaomrai Rais Ruto kurejelea mfumo wa zamani (DUC). Wanadai kuwa mfumo mpya wa ufadhili wa wanafunzi katika vyuo vikuu unawabagua wanafunzi maskini.

Hata hivyo, manaibu wa chansela wakiongozwa na Maprofesa Laban Ayiro (Daystar), Samuel Gudu (Rongo), Emily Achieng (Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Jaramogi Oginga Odinga), Laila Abubakar (Technical University of Mombasa), Aloo Obudho (Maasai Mara) wamesema mfumo mpya ni nzuri na utamaliza umaskini ambao umekuwa ukigubika vyuo vikuu nchini.

Wakizungumza wakati wa mkutano wa Baraza la Mtandao wa Viongozi wa Taasisi za Kibiashara (KNEIL) uliofanyika Mombasa, wasimamizi hao waliwahimiza wazazi na wanafunzi kuunga mkono mpango huo wa ufadhili.

“Mpango wa kufadhili vyuo vikuu ni jaribio la kutatua tatizo, kama Wakenya tunapaswa kufurahia hilo. Mpango huu ni sharti upatiwe muda wa kukua na kisha tutaona sehemu zake anuai zinazohitaji kuangaziwa upya,” alisema Profesa Ayiro.

Alisema tangazo la Rais kuwa serikali itaingilia kati kulinda vyuo vikuu wakati huu wa mageuzi litainua taasisi hizo.

“Nilikuwa na fursa ya kuwa naibu chansela katika chuo kikuu cha umma, nafikiri hatujatumia kikamilifu uwezo wa kuzalisha mapato ambao vyuo vyetu vinajivunia,” alisema.

Msimamizi huyo wa chuo kikuu alihimiza vyuo vikuu kutumia nafasi zilizopo za biashara, ubunifu na mauzo ili kuongeza mapato badala tu kutegemea karo ya wanafunzi.

Alisema kuna raslimali nyingi duniani zinazoweza kutumiwa kuhakikisha taasisi za elimu ya juu hazitegemei Hazina ya Kitaifa pekee kupata msaada kwa bajeti zake za maendeleo .

Kulingana naye, mfumo wa zamani haukufaa kwa sababu vigezo muhimu havikuzingatiwa.

Kwa upande wake, Profesa Gudu alisema mfumo huo utaokoa taasisi za elimu ya juu ambazo zimekuwa ziking’ang’ana na changamoto za kifedha.

“Tunapaswa kutekeleza mfumo mpya ili kutatua changamoto,” alisema Profesa Gudu.

Mkurugenzi wa Shirika la Kitaifa kuhusu Ubunifu, Dkt Tonny Omwansa amehimiza vyuo vikuu kufanya kazi pamoja ili kubuni suluhisho kwa jamii.

Profesa Abubakar, ambaye vilevile ni mwanachama wa Jopokazi la Rais kuhusu Mageuzi ya Elimu, aliunga mkono mfumo mpya akiutaja kama unaopatia wanafunzi kipaumbele japo akasema utekelezaji wake ndio haujafanikiwa.

“Sisi ndiyo tulipendekeza mfumo huo wa ufadhili ila tatizo ni utekelezaji wake. Serikali ilistahili kulipa vyuo vikuu asilimia 80 na wazazi wakilipa asilimia 20,” akasema Profesa Abubakar.

Manaibu chansela pia walitetea mfumo huo wakisema kuwa washikadau walilenga kuhakikisha kuwa wazazi pia wanamegewa mzigo wa kufadhili gharama ya elimu ya juu.