Habari za Kitaifa

Lenolkulal nje kwa dhamana ya Sh10 milioni

Na RICHARD MUNGUTI August 31st, 2024 2 min read

MAHAKAMA kuu imewaachilia kwa dhamana ya Sh10milioni aliyekuwa Gavana wa Samburu Moses Lenolkulal na mfanyabiashara Hesbon Ndathi waliofungwa Alhamisi Agosti 29,2024 kwa kupokea kwa njia ya ufisadi Sh83,460,995.

Lenolkulal alitozwa faini ya Sh85,460,995 ama atumikie kifungo cha miaka minane jela ilhali Ndathi alitozwa faini ya Sh83,460,995.

Wawili hawa walikuwa hawajalipa faini hiyo ya jumla ya Sh168,821,990.

Waliachiliwa kutoka gereza la Viwandani Ijumaa alasiri baada ya kulipa dhamana hiyo ya Sh10m kila mmoja.

Hakimu mkuu mahakama ya kuamua kesi za ufisadi  Thomas Nzioki aliamuru Lenolkulal, Ndathi na maafisa wa zamani wa kaunti hiyo wasichaguliwe wadhifa wowote wa umma  kwa muda wa miaka 10.

Wafungwa wenzao 8 walitozwa faini ya Sh6.6milioni ama kutumikia kifungo cha miaka  minne kila mmoja.

Lenolkulal na Ndathi  waliachiliwa na Jaji Diana Kavedza wa Mahakama Kuu , Kibera kwa dhamana ya  Sh10milioni  na mdhamini mmoja wa kiasi na hicho.

Jaji Kavedza aliamuru rufaa iliyowasilishwa na wakili

itajwe October 31, 2024 ili kutengewa siku ya kusikizwa.

Lenolkulal na Ndathi walipinga uamuzi wa hakimu mkuu mahakama ya kuamua kesi za ufisadi Milimani Thomas Nzioki wakisema alipotoka kisheria alipoifikia uamuzi kwamba walijinufaisha na pesa za umma Sh83,460,995.

Wawili hawa wanasema Nzioki alipotoka na kukosea alipofikia uamuzi kwamba waliilaghai kaunti hiyo pesa ilihali ilipokea mafuta na kulipa kampuni ya Oryx Service Station.

Aliyekuwa Gavana wa Samburu Moses Kasaine Lenolkulal (kushoto) na Stephen Letinina waliofungwa jumla ya miaka 12 kwa ufisadi. PICHA | RICHARD MUNGUTI

Lenolkulal alijitetea akisema hana hatia na kwamba alikuwa ameandikia kaunti hiyo barua Aprili 5, 2013 akifichua kwamba kampuni ya Oryx itakuwa inathibitiwa na Ndathi.

“Ndathi na Lenolkulal walikuwa na uhusiano wa karibu. Lenolkulal alijiondoa katika uendelezaji wa biashara ya kuuzia mafuta kaunti ya Samburu na kumpisha Ndathi. Ukweli ni kwamba alijificha nyuma ya Ndathi. Lenolkulal ndiye alikuwa akifanya biashara na kaunti aliyokuwa Gavana,” Nzioki alisema.

Katika rufaa yao wafungwa hao walisema hakimu alipotoka kufikia uamuzi  waliilaghai kaunti pesa.

Jaji Kavedza aliamuru kesi hiyo itajwe mbele ya mahakama ya Milimani kwa maagizo zaidi.

Lenolkulal na Ndathi walikata rufaa kupinga adhabu watumikie kifungo kwa kujinufaisha na pesa za umma kati ya 2013 na 2019.

Kampuni ya Oryx iliyoandikishwa na Lenolkulal kabla ya kuchaguliwa kuwa gavana  ilishinda zabuni ya kuuzia kaunti ya Samburu mafuta ya petroli.