Habari za Kitaifa

Mganga Mtanzania atapeli Wakenya Sh104 milioni kufukuza mapepo

Na BRIAN OCHARO September 1st, 2024 2 min read

FAMILIA moja Mombasa imeachwa ikikuna kichwa baada ya raia wa Tanzania kuwatapeli zaidi ya Sh104 milioni katika mpango uliokusudiwa kuwakomboa kutoka katika utumwa wa mapepo.

Bw Mahendra Kumar na Bw Bhavir Kumar waliripotiwa kupoteza mamilioni ya pesa kwa Bw Sadiki Jumanne Nyarembe, ambaye alipaswa kufukuza mapepo kutoka kwa familia yao na kutakasa mali yao kutokana na mapepo chafu.

Wapelelezi walidai kuwa utapeli huu ulifanyika kati ya Januari na Agosti 2024 .

Utapeli huu ulibainika kufuatia kukamatwa kwa Bw Nyarembe katika eneo la Nyali ambapo ilipatikana hakuwa na hati muhimu za kusafiri mnamo Agosti 28.

Siku iliyofuata, Bw Nyarembe alifikishwa mbele ya mahakama ya Mombasa, ambapo serikali ilimfungulia mashtaka kadhaa.

Wapelelezi bado wanawasaka washirika wake, ambao wanadai alipanga nao njama ya kulaghai familia hiyo mamilioni ya pesa.

Raia huyo wa Tanzania anadaiwa kuwahadaa Bw Mahendra na Bw Bhavir kwamba walikuwa na mapepo chafu na kwamba alikuwa na uwezo wa kuyafukuza mapepo hayo na pia kutakasa mali yao.

Bw Nyarembe anakabiliwa na makosa manne, ikiwemo kupanga njama ya utapeli, kujipatia hela kwa njia za uongo, na kupatikana nchini Kenya kinyume cha sheria.

Katika shtaka la kwanza, Bw Nyarembe alishtakiwa kuwa katika tarehe na saa isiyojulikana, alipanga njama na watu wengine ambao bado hawajakamatwa, kuwatapeli Bw Mahendra na Bhavik kwa kuwahadaa kuwa wana mapepo.

Mahakama iliambiwa kwamba mshukiwa alitumia udanganyifu huu kufanya tambiko la kutoa, mapepo kwa waathiriwa wake.

Ilidaiwa kuwa aliwapotosha wakaamini kuwa walikuwa na pepo chafu.

Katika shtaka la pili, Bw Nyarembe alishtakiwa kwa kupokea Sh101.5 milioni kutoka kwa Bw Mahendra kwa kudai kuwa angefanya ibada ya kufukuza mapepo ili kuikomboa familia ya mwathiriwa kutokana na mapepo hao.

Katika shtaka la tatu, mahakama ilielezwa kwamba mshukiwa alijipatia vito vya dhahabu vya thamani ya Sh3 milioni kutoka kwa mwathiriwa kwa madai ya uongo kwamba angevitakasa pepo mbaya. Inadaiwa alitenda kosa hili saa mbili usiku Februari 12, 2024.

Bw Nyarembe pia alishtakiwa kwa kuwa nchini Kenya kinyume cha sheria, ambapo serikali ilifahamisha mahakama kuwa alipatikana nchini bila hati zozote za kusafiria.

Mahakama iliambiwa kwamba mshukiwa alipatikana eneo la Nyali mnamo Agosti 20, 2024, bila hati sahihi za kusafiria zinazomruhusu kukaa Kenya kihalali.

Bw Nyarembe, hata hivyo, alikanusha mashtaka yote alipofika mbele ya Hakimu Mkuu Mkazi Gladys Olimo.

Hakimu aliamuru mshukiwa aachiliwe kwa dhamana ya Sh15 milioni, bila mbadala ya pesa taslimu.

Pia, mshukiwa huyo anatakiwa kutoa wadhamini wawili wa Kenya kando na dhamana ya Sh15 milioni kwa vile yeye ni raia wa kigeni.

Bw Nyarembe pia aliagizwa kuweka hati yake ya kusafiria mahakamani kabla ya kupata uhuru wake akitimiza masharti ya dhamana aliyowekewa.

Mahakama iliweka masharti hayo magumu ya dhamana baada ya Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP), kupitia kwa kiongozi wa mashtaka Alex Gituma, kumtaka hakimu kuzingatia kwamba Bw Nyarembe alikuwa mgeni.

Upande wa mashtaka pia uliiomba mahakama kuzingatia kiasi cha pesa ambacho kinadaiwa kupotea katika utapeli huo.