Habari za Kitaifa

Mkenya mtoro anayedaiwa kuangamiza mpenziwe kushtakiwa Amerika 

Na HILLARY KIMUYU na RICHARD MUNGUTI September 3rd, 2024 Kusoma ni dakika: 2

MKENYA anayeshukiwa kuua mpenzi wake Amerika Oktoba 31, 2023, amerejeshwa kimabavu jijini Massachusetts ambapo atafunguliwa mashtaka ya mauaji hii leo, Jumanne, Septemba 3, 2024.

Taarifa kutoka kwa Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP), ilisema Kevin Kang’ethe — aliyewahi kuwa mtoro baada ya kutoweka Amerika na baadaye kutoroka Kituo cha Polisi cha Muthaiga, aliondoka Kenya Jumapili, Septemba 2, 2024.

“Hatua hiyo imejiri baada ya DPP Renson Ingonga kumhakikishia Mkurugenzi wa FBI, Christopher Wray…kuwa afisi yake imejitolea kuhakikisha haki imetekelezwa upesi kuhusu kisa hicho,” ilisema taarifa.

“Kwa familia ya marehemu Margaret Mbitu, tunawaahidi msaada wetu na kusimama nanyi kwa maombi,” alisema Bw Ingonga.

Bw Kang’ethe, 40, anadaiwa kumuua mpenzi wake Margaret Mbitu, msaidizi wa kutoa huduma ya afya nyumbani mjini Halifax, Massachusetts — kati ya Oktoba 30 na Novemba 1, 2023.

Kisha alikimbilia Kenya, na kibali cha kumkamata kikatolewa na Korti ya jimbo la Chelsea, Massachusetts, kilichofuatiwa na ombi alilotumiwa Bw Ingonga la kumrejesha mshukiwa.

Alikamatwa Januari 30, 2024, eneo la Parklands, Kaunti ya Nairobi lakini akatoweka kizuizini kabla ya kukamatwa tena.

Ushahidi unaonyesha Kang’ethe alimshambulia kikatili kwa kumdungadunga Mbitu mara kadhaa usoni na shingoni hadi akafa.

Mbitu alitoweka Oktoba 30, 2023, baada ya kutoka kazini mwake ambapo familia yake, baada ya kumsaka bila mafanikio, iliandikisha taarifa katika Kituo cha Polisi cha Whitman walioshirikisha Kituo cha Polisi cha Massachusetts.

Uchunguzi wa awali ulionyesha aliondoka kazini pake na kusafiri pamoja na Kang’ethe hadi alipokuwa anaishi mjini Lowell.

Baada ya kukamatwa mara ya kwanza Kenya, Kang’ethe alitoweka Kituo cha Polisi cha Muthaiga kwa njia ya kutatanisha.

Polisi walisema alitoweka walipokuwa kwenye mkutano na mwanamume aliyedai kuwa wakili wake.

Alipokuwa mafichoni, inasemekana familia yake ilishiriki kikao na uamuzi ukafanywa kumfichua au kutoa ripoti kwa polisi ikiwa angemwendea yeyote baina yao.

Mtoro alipowasili katika nyumba ya kukodisha ya binamu yake, jamaa wa familia walidokezea polisi.

“Hatungemruhusu kuondoka tena kwa sababu kutoweka kwake korokoroni, kulikuwa kunawasababishia masaibu watu wengi.

“Kwa sababu sisi ni raia wanaozingatia sheria, tulikuwa tayari tumeamua ikiwa yeyote atampata, basi tutamsalimisha,” jamaa wa familia yake alieleza Taifa Dijitali wakati huo.

Imetafsiriwa na Mary Wangari