Habari za Kitaifa

Makachero wanasa maelfu ya lita za kemikali hatari ya ethanol

Na KEVIN CHERUIYOT September 3rd, 2024 1 min read

MAKACHERO kutoka Mamlaka ya Kukusanya Ushuru (KRA) na Idara ya Kuchunguza Uhalifu (DCI) wamekamata trela mbili zilizokuwa zinasafirisha kemikali inayofahamika kama ethanol kutoka Uganda kuelekea Limuru.

Haya yamejiri wakati ambapo taifa bado linapambana na pombe haramu inayoundwa kutokana na kemikali ya ethanol inayouzwa kimagendo, na kusababisha ushindani usio wa haki kibiashara na kuhatarishia Wakenya afya zao.

Tukio hilo limefichua njama mpya zinazotumiwa na wafanyabiashara wakora kukwepa serikali kwenye vituo vya mpakani ili kuendeleza ulanguzi wa ethanol.

Kufuatia uchunguzi uliojumuisha vikosi mbalimbali, iligunduliwa kuwa tanka mbili zilizokuwa zimewekwa alama ya kusafirisha bidhaa za sukari zilikuwa zimeficha lita 40,971 za ethanol ya magendo yenye thamani ya Sh26.9 milioni.

“Kemikali hiyo ya ethanol ilikuwa inasafirishwa kuelekea Limuru katika matanka mawili ya trela zilizobeba lita 17,766 na lita 23,205 lita na zilizovuka kuingia Kenya kupitia mpaka wa Lwakhakha kati ya Agosti 19 na 24, 2024,” ilisema KRA.

Kulingana na ripoti hiyo, vijisehemu vya matanka hayo mawili vilikuwa vimejazwa jumla ya lita 2,720 pekee za molasi huku nyingine zikijumuisha vijisehemu vilivyofunikwa na kujazwa ethanol.

“Vifuniko vya matanka hayo viliundwa kutoa molasi huku ethanol, ambayo ina uzito, ikisalia kufichwa na inaweza tu kutolewa kwa kutumia mifereji inayopitishwa kwenye vijisehemu hivyo vilivyofichwa.”

Magari hayo mawili yalichunguzwa ili kufichua vijisehemu hivyo vilivyofichwa kabla ya kupeleka bidhaa zilizopatikana kufanyiwa vipimo ili kuonyesha kemikali zilizopo.

Oparesheni hiyo ilianza Jumapili, Agosti 25 hadi Jumatano wiki iliyopita ambapo ethanol ilipatikana.

Kulingana na maafisa, trela hizo zilifuatwa kutoka mpakani hadi kituo chake ambapo dereva kwa jina, Edward Nandwa Otundo, alikamatwa katika oparesheni hiyo huku mwingine akifanikiwa kutoweka.

“Bidhaa hizo kwa sasa zimezuiliwa katika bohari ya KRA huku uchunguzi ukifanyika na washukiwa kufunguliwa mashtaka. Habari zilizopo zinaashiria trela zote mbili zinamilikiwa na Isaac Muigai Kahugu.”

Mshukiwa aliyekamatwa amerushwa korokoroni huku polisi wakiendelea kumsaka dereva aliyetoweka na mmiliki wa tankan na shehena hiyo.

Imetafsiriwa na Cecil Odongo