Habari za Kitaifa

Sababu za Shilingi ya Kenya kubakia imara mashirika yakishusha hadhi ya Kenya

Na BENSON MATHEKA September 4th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

SHILINGI ya Kenya ilibaki thabiti, ikibadilishwa kwa Sh129.25 kwa Dola ya Amerika licha ya nchi kushushwa hadhi kiuchumi na mashirika ya kimataifa yanayokadiria uwezo wa kulipa madeni.

Wachambuzi wa kimataifa walisema hii inatokana na mahitaji na usambazaji wa Dola na hatua zilizochukuliwa na Benki Kuu ya Kenya.

Kulingana na wataalamu, mahitaji ya Dola ya sekta ya viwanda yanalingana na fedha za kigeni zilizoingia nchini kutoka kwa wawekezaji wa kigeni ambao walitaka kununua bondi za miundombinu za serikali na uamuzi wa Benki Kuu kununua Dola ili kuzuia kuyumba kwa sarafu ya nchi.

Kufikia Ijumaa wiki jana, Agosti 30, 2024 benki za biashara zilibadilisha Dola ya Amerika kwa shilingi 129.25 ilivyokuwa Alhamisi.

Hata hivyo, siku ya Jumatano shilingi ya Kenya iliimarika kidogo hadi Sh129.50 ikilinganishwa na Sh129.25 siku iliyotangulia.

Hii ilitokana na mapato ya Dola kutoka sekta ya kilimo na uamuzi wa Benki Kuu kununua Dola ili kuzuia kuyumba kwa sarafu ya Kenya.

Shilingi imekuwa thabiti kwa miezi kadhaa tangu Februari, na hivyo kupunguza wasiwasi kwamba nchi hii yenye uchumi thabiti zaidi Afrika Mashariki, itashindwa kulipa deni la Sh310 bilioni ambalo muda wake wa kulipiwa ulifika Juni.

Hali ya hivi punde ya shilingi inajiri siku chache baada ya wachambuzi kufichua kuwa sarafu ya Kenya ingebaki thabiti kutokana na ongezeko la imani ya wawekezaji kwa nchi baada ya maandamano ya Gen Z.

Shilingi ya Kenya pia ilitarajiwa kubaki thabiti kufuatia kupungua kwa mahitaji ya fedha za kigeni.

Kulingana na wataalamu, shilingi ingetulia kidogo dhidi ya Dola baada ya wazalishaji na waagizaji wa mafuta kuamua kupunguza ununuzi wao wa Dola.

Hata hivyo, shilingi inasalia kuwa sarafu inayofanya vizuri zaidi duniani baada ya thamani yake kuongezeka kwa takriban asilimia 17 dhidi ya Dola.

Hii ni licha ya kudorora mapema Julai 2024 kufuatia kushushwa hadhi kwa nchi na shirika la ukadiriaji wa mikopo la Moody hadi kiwango cha ‘Caa1’ kutoka ‘B3’.

Kushushwa hadhi kwa Moody kulichangiwa na hofu kuwa nchi ingeshindwa kulipa madeni yake ya nje kutokana na sera mbovu za kifedha za Kenya pamoja na maandamano ya hivi majuzi dhidi ya serikali.