Wafugaji kupokea mafunzo kufuatia mlipuko wa maradhi
KAUNTI ya Kirinyaga imezindua kampeni kuhamasisha wafugaji kuhusu magonjwa ya mifugo kufuatia kuripotiwa kwa kisa cha ugonjwa wa Mguu, Mdomo na Ngozi eneo hilo.
Kampeni hiyo inanuiwa kuwapa wakulima maelezo muhimu kuhusu kuzuia, kugundua na kudhibiti ugonjwa huo.
Waziri wa kaunti hiyo anayehusika na Kilimo, Ufugaji na Uvuvi, Dkt John Gachara, alisema mafunzo hayo yamejiri kufuatia mlipuko wa maradhi ambao sasa umedhibitiwa.
“Baadhi ya wakulima wamekuwa wakisema kuwa wanarekodi visa vya ugonjwa wa Ngozi iliyokunjana na Mguu na Mdomo na maafisa wetu walipokwenda mashinani, tuligundua suala kuu ni kukosa maarifa ya kutosha kuhusu kuzuia na kugundua maradhi hayo,” alisema Dkt Gachara.
Alisema wahudumu kutoka vituo vya kibinafsi, maafisa wa umma kutibu mifugo na maafisa kutoka vyama vya ushirika vya wafugaji wa ng’ombe wa maziwa pia wamepokea mafunzo ili kuwawezesha kuchukua hatua za dharura kuhusu magonjwa yanapozuka.
“Serikali ya Kaunti pamoja na wadau katika sekta ya ufugaji wa ng’ombe wa maziwa wameweza kubuni mpango wa kuwaelimisha wafugaji unaoendeshwa katika wadi zote na maafisa wetu,” alisema.