Waziri Murkomen aongoza jamii ya wanamichezo Kenya kuomboleza mwanariadha wa Uganda Rebecca Cheptegei aliyeaga dunia
WAZIRI wa Michezo, Kipchumba Murkomen ameongoza jamii ya wanamichezo nchini kuomboleza mwanariadha wa Uganda ambaye pia ni Mkenya, Rebecca Cheptegei, aliyeaga dunia mapema leo, Alhamisi, Septemba 5, 2024.
Bi Cheptegei alikuwa amelazwa katika Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Moi, (MTRH), Eldoret, Kaunti ya Uasin Gishu alikokuwa akipokea matibabu kufuatia majeraha aliyouguza baada ya kuvamiwa mchumba wake wa zamani.
Waziri Murkomen alimtaja Cheptegei kama mwanariadha mashuhuri ambaye alitumia kipaji chake kuiwakilisha nchi ya Uganda na Afrika Mashariki katika Olimpiki.
“Ni jambo la kusikitisha kuskia kifo cha mwanariadha huyo aliyekuwa akiiwakilisha nchi yake na Afrika Mashariki katika michezo,” akasema Bw Murkomen.
Kando na hayo, alisema kuna haja suala la dhuluma dhidi ya wanawake lishughulikiwe ipasavyo kwani linaendelea kuandikisha visa vya kuhuzunisha katika jamii akirejelea kisa kilichomtendekea mwanariadha huyo, aliyeshambuliwa na mpenzi wake wa zamani.
Habari za kifo chake zilitolewa na uongozi wa hospitali hiyo na kuthibitishwa na familia yake.
“Bi Rebecca aliaga dunia wakati akipokea matibabu kutokana na majeraha aliyopata baada ya kuvamiwa na mpenziwe wa kitambo,” familia yake ilisema.
Mshukiwa, anasemekana kummwagilia mafuta ya petroli na kumteketeza kwa moto, ambapo inasemekana aliuguza majeraha zaidi ya asilimia 80 mwilini mwake.
Cheptegei, mwenye umri wa miaka 33, aliungua vibaya kutokana na makali ya moto.
Serikali ya Kenya mnamo Septemba 4, 2024 ilisema kwamba maandalizi yalikuwa yanaendelea kumsafirisha Cheptegei hadi Nairobi kwa matibabu maalum, lakini hilo halikufanikishwa.
Kulingana na Katibu Mkuu wa Michezo, Peter Tum, alifichua kuwa kumekuwa na mazungumzo na Waziri wa Michezo wa Uganda, Peter Ogwang, na makubaliano yaliafikiwa ya kumsafirisha kwa ndege hadi Nairobi kwa matibabu na kumpa matunzo maalum.
Rais wa Riadha nchini Kenya, Jack Tuwei, alikashifu tukio hilo akisema halipaswi kutokea kwa mtu yeyote kwa sababu maisha ni ya thamani na lazima yaheshimiwe kila wakati, akiongeza kuwa watu wanapaswa kuishi kwa amani kila wakati.
“Tukio lililompata mwanariadha wetu kutoka Uganda, kwa kweli ni la kusikitisha kwa sababu huwezi kumdhuru mtu kwa ajili hamjaelewana kuhusu masuala ya ugavi wa mali. Kama shirikisho, tunataka kulaani tukio hilo, hatupaswi kuishi hivyo,” alisema Tuwei, ambaye pia ni makamu wa rais wa IAAF.