Habari

Rais Ruto aagiza uchunguzi ufanywe kuhusu vifo shuleni na waliohusika wachukuliwe hatua

Na BENSON MATHEKA September 6th, 2024 1 min read

IDADI ya wanafunzi waliofariki katika mkasa wa moto ulioteketeza bweni la Shule ya Hillside Endarasha Academy, Kaunti ya Nyeri imefikia 17

“Tunafariji familia za watoto waliopoteza maisha yao katika mkasa wa moto katika shule ya Hillside Endarasha Academy Kaunti ya Nyeri,” Rais Ruto alisema katika ujumbe aliotuma kutoka China.

Alisema kuwa wizara ya usalama wa ndani itafanya kila juhudi kusaidia familia zilizoathirika.

Msemaji wa Huduma ya Kitaifa ya Polisi Dkt .Resila Onyango alisema timu ya maafisa wa uchunguzi imetumwa katika shule hiyo iliyoko eneobunge la Kieni, Kaunti ya Nyeri.

Wanafunzi 16 walithibitishwa kufariki ndani ya bweni na mmoja akafariki alipofikishwa hospitalini.

“Kumi na sita walichomeka kiasi cha kutotambuliwa huku mmoja akifariki akipelekwa hospitalini,” Msemaji wa polisi aliambia Nation FM.. Tunachunguza kilichosababisha moto huo na tutachukua hatua zinazohitajika,” alisema.

Timu ya wachunguzi inaongozwa na Naibu Mkurugenzi wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI), John Onyango, na maafisa kutoka Afisi ya Inspekta Jenerali wa Polisi.

“Moto ulizuka katika bweni, Ulizuka usiku na bado hatujabaini kilichousababisha,” alisema Dkt Onyango.

Kuna hofu kuwa huenda idadi ya waliokufa ikaongezeka huku wanafunzi 14 wakilazwa hospitalini.