Masengeli akohoa, aapa kuzima ulanguzi wa dawa za kulevya
KAIMU Inspekta Jenerali wa Polisi Gilbert Masengeli amewaonya walanguzi wa dawa za kulevya katika eneo la Pwani akihoji kuwa idara ya polisi iko tayari kupambana kikamilifu na janga hilo kama njia ya kuhakikisha vijana na wakazi wa Pwani wako salama.
Akizungumza katika ziara yake Kaunti ya Mombasa baada ya kukutana na maafisa wa usalama eneo la Pwani, alieleza kuwa mikakati kabambe ilikuwa imewekwa kukamata walanguzi ili wafkishwe mahakamani.
“Tumekuwa hapa Pwani kwa ziara maalum ambayo ililenga kuhakikisha kuwa hali ya usalama eneo la Pwani inaimarishwa. Nafahamau kuwa suala la Mihadarati ni donda sugu hapa. Ninawaonya hao walanguzi wanaotupatia shida, polisi watawakamata na kufikishwa mahakamani,” akaonya Bw Masengeli.
Aidha, Bw Masengeli alidokeza kuwa, kulikuwa na juhudi kabambe kupambana ipaswavyo na wahalifu wanaotumia bodaboda kuwaibia simu wakazi.
Kwa mujibu wake, wakati wao ulikuwa umefikia mwisho kwani maafisa walikuwa wamejiandaa kuwakabili.
“Wengi wa hawa wezi wa simu wanaosumbua umma hapa Pwani tunawachunguza. Tayari tushawashika wahalifu kadhaa na tutawafikisha mahakamani. Kwa wale ambao hawajashikwa wafahamu tunaendelea na uchunguzi wetu na hivi karibuni tutawapata,” akasema Bw Masengeli.
Licha ya hayo, Bw Masengeli aliomba kutozungumzia suala la kukiuka amri ya Mahakama kumtaka kufika mbele yake kueleza kupotea kwa wanaharakati watatu, akisema kuwa jambo hilo lilikuwa mbele ya mahakama na kwa hivyo hakuruhusiwa kutoa maoni kulihusu.