Habari za Kitaifa

Wazazi washauriwa wasitume watoto wachanga shule za bweni

Na WINNIE ONYANDO September 8th, 2024 1 min read

RAIS wa Bunge la Mwananchi, Francis Awino, amewashauri wazazi kuepuka kuwapeleka watoto wao wenye umri mdogo katika shule za bweni.

Akirejelea mkasa wa moto uliotokea katika Shule ya Hillside Endarasha Academy, iliyoko Kieni, Nyeri na kuwauwa wanafunzi 21, Bw Awino alisema kuwa kuwapeleka watoto wenye umri mdogo katika shule za bweni ni kuhatarisha maisha yao.

“Ni jambo la kusikitisha sana kuwaona watoto wetu wakiangamia kwenye mkasa kama huo. Ila ushauri wangu ni kuwa wazazi hawafai kuhatarisha maisha ya watoto wao kwa kuwapeleka katika shule za bweni wakiwa na umri mdogo,” Bw Awimo aliambia Taifa Dijitali.

Kulingana na yeye, wazazi wanafaa kusubiri hadi mtoto aingie katika shule ya upili ndipo apelekwe katika shule ya bweni.

“Mtoto wa shule ya upili anaweza kujitegemea na kujiokoa wakati wa mkasa,” akaongeza.

Haya yanajiri siku chache tu baada ya taifa kuamkia taarifa za kusikitisha kufuatia mkasa wa moto ulioangamiza wanafunzi 21.

Rais William Ruto pia aliagiza uchunguzi ufanywe kuhusiana na mkasa huo na wahusika wachukuliwe hatua za kisheria.

“Tunafariji familia za watoto waliopoteza maisha yao katika mkasa wa moto katika shule ya Hillside Endarasha Academy Kaunti ya Nyeri,” Rais Ruto alisema katika ujumbe aliotuma kutoka China.

Alisema kuwa wizara ya usalama wa ndani itafanya kila juhudi kusaidia familia zilizoathirika.

Timu ya wachunguzi ikiongozwa na Naibu Mkurugenzi wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI), John Onyango, na maafisa kutoka Afisi ya Inspekta Jenerali wa Polisi wanaendelea na uchunguzi.