Magut, Jerotich watamba Nairobi City Marathon
WAKIMBIAJI Eliud Magut na Cynthia Jerotich wameibuka washindi wa mbio za kilomita 42 kwenye mashindano ya Nairobi City Marathon jijini Nairobi, Jumapili, Septemba 8.
Katika makala hayo ya tatu yaliyovutia washiriki 15,000, Magut alitawala kitengo cha wanaume cha 42km kwa saa mbili, dakika tisa na sekunde 47, akifuatwa kwa karibu na Josphat Bett (2:10:01) na Emmanuel Sikuku (2:10:05) katika usanjari huo.
Jerotich ametumia saa 2:28:02 kubeba taji la wanawake baada ya kumaliza umbali wa 42km mbele ya Lilian Chebii (2:28:02) na Peris Jerono (2:28:29), mtawalia.
Robert Kiprop (1:00:56) na Marion Kibor (1:08:55) walitetemesha katika mbio za 21km, wakimaliza vitengo vya waunaume na wanawake kwa 1:00:56 na 1:08:55, mtawalia.
Mbio za kilomita 10
Amos Kipkemoi na Edna Kibiwot waliponyoka na mataji ya 10km kwa dakika 29:04 na 33:25, mtawalia.
Kiprop alifuatwa unyo kwa unyo na Wilson Too (1:01:14) na Timothy Kibet (1:01:25) naye Kibor alikamilisha mbele ya Gladys Chepkurui (1:09:04) na Sharon Kiptugen (1:09:27).
Kipkemoi alimpiku mpinzani wake wa karibu Filex Kibet (29:13) na Gideon Kipngetich (29:16) nao Fridah Ndinda (34:12) na Naomi Tigoi (34:22) wakafunga tatu-bora katika 10km za wanawake.
Waziri wa Michezo Kipchumba Murkomen alishiriki kitengo cha 10km.
Washindi wa makala ya 2023 Robert Kiplimo na Naom Jebet (42km), Maxwell Rotich kutoka Uganda na Gladys Chepkurui (21km) pamoja na Peter Aila na Brenda Tuwei (10km) waliingia makala ya mwaka huu wakilenga kuhifadhi mataji yao, lakini wakazidiwa maarifa.
Makala ya mwaka huu yalihudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiongozwa na Bw Murkomen.