Jamvi La SiasaMakala

Gachagua alilia umoja Mlima Kenya huku uhasama na Kindiki ukifufuka

September 11th, 2024 Kusoma ni dakika: 3

UHASAMA wa kisiasa kati ya Naibu Rais Rigathi Gachagua na Waziri wa Usalama wa Ndani Prof Kithure Kindiki umefufuka na kutishia umoja wa eneo la Mlima Kenya.

Tofauti kati ya wawili hao zilidhihirika wakati wa uteuzi wa mgombea mwenza wa Dkt William Ruto kabla ya uchaguzi wa 2022 na zinaweza kuendelea hadi uchaguzi mkuu ujao.

Vita vyao vya ubabe vimegawanya Mlima Kenya Mashariki anakotoka Profesa Kindiki na Mlima Kenya Magharibi anakotoka Bw Gachagua wakati ambao uhusiano kati ya Rais Ruto na Bw Rigathi Gachagua unasemekana kuingia baridi.

Matukio ya hivi punde ambayo yalishuhudia kundi la wabunge kutoka Mlima Kenya Mashariki kujitenga na kumuidhinisha Prof Kindiki kama msemaji wao yanaonekana kuwa mpango wa kupunguza ushawishi wa naibu rais iwapo atafaulu kuondoa Mlima Kenya kutoka UDA.

Wabunge 14 kutoka kaunti za Tharaka Nithi, Meru na Embu Jumatatu walielezea nia ya kujitenga na kaunti za magharibi zinaojumuisha Murang’a, Nyeri, Kiambu, Nyandarua, Laikipia, Kirinyaga, Nairobi na Nakuru.

Bw Gachagua alikuwa akijikuna kichwa kujaribu kuzima mpasuko huo akiwa na aliyekuwa rafiki yake aliyegeuka mpinzani mkuu, Bw Kenyatta, ambaye walitofautiana naye 2022 baada ya kumuidhinisha Dkt Ruto kuwania urais dhidi ya mwaniaji anayependekezwa na rais huyo mstaafu, kinara wa upinzani Raila Odinga. .

Bw Gachagua alimuomba msamaha hadharani Bw Kenyatta akitaka kuungana naye ili kujipiga jeki katika vita vya ubabe na mrengo wa rais katika UDA eneo la Mlima Kenya lakini bado hajafaulu.

Matatizo ya Bw Gachagua yameongezeka baada ya Rais Ruto kuungana kisiasa na Bw Odinga. Tayari anapigana na washirika wa rais katika Mlima Kenya wakiongozwa na Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa Kimani Ichungwah na Mbunge wa Laikipia Mashariki Mwangi Kiunjuri, na kujitenga kwa kambi ya mashariki, au uasi wa viongozi kutoka eneo hilo, kutaongeza upinzani.

Gavana wa Nyeri Bw Mutahi Kahiga alipuuzilia mbali hatua hiyo akisema ni upuzi tu.

Bw Kahiga alisema anashuku hatua hiyo kuwa sehemu ya mpango mpana wa kugawanya eneo hilo kabla ya uchaguzi mkuu wa 2027.

‘Wabunge hawa wote wanaosema wanataka kugawanya Mlima Kenya ndio waliopiga kura ya ndiyo kwa Mswada wa Fedha wa 2024 dhidi ya matakwa ya watu wengi,’ gavana alisema, na kuongeza kuwa ‘huhitaji ushahidi zaidi kwamba hili ni tamko kutoka kwa watu ambao hawasikizi raia mashinani.’

Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Kikuyu Bw Wachira Kiago mnamo Jumatatu alipuuzilia mbali hatua ya kujitenga kwa eneo la mashariki akisema ni matokeo ya mizozo isiyo ya busara ya wanasiasa inayolenga kuendeleza migawanyiko.’

‘Kama vile unavyohitaji kura ya maoni ili kubadilisha mipaka ya kitaifa, unahitaji mashauriano zaidi ili kupata uamuzi wa kubadilisha Mlima Kenya kisiasa,’ alisema.

Bw Kiago alisema ushindani wa kisiasa unaoendelea katika eneo la Mlima Kenya unageuka kuwa mbaya kwa watu wa eneo hilo ambao badala ya kuhudumiwa kulingana na ahadi za kabla ya uchaguzi mkuu, wanazungushwa tu.

Katika kikao na wanahabari siku ya Jumatatu, viongozi wa Mlima Kenya Mashariki kupitia Mbunge wa Mbeere Geoffrey Ruku walisema sasa wanamtambua Bw Kindiki kuwa msemaji wao. ‘Kama wabunge wa Mlima Kenya mashariki, na kwa niaba ya watu wetu, tumekubaliana kwa kauli moja kwamba msemaji wetu ni Prof Kindiki,’ walisema.

Viongozi hao walifanya uamuzi huo katika mkutano wa bunge uliofanyika katika hoteli moja mjini Embu.

Walisema eneo lao limewakilishwa katika serikali kupitia Mawaziri Kindiki, Justin Muturi (Utumishi wa Umma) na Eric Mugaa (Maji na Usafi wa Mazingira).

Waliohudhuria mkutano huo ni wabunge Ruku (Mbeere Kaskazini), Mpuru Abuuri (Tigania Mashariki), Elizabeth Karamu (Mwakilishi wa wanamke Meru), John Mutunga (Tigania Magharibi), John Paul Mwirigi (Igembe Kusini), Seneta Alexander Mudigi (Embu), Dan Kiili (Igembe ya Kati), Gitonga Murugara (Tharaka), Pamela Njoki (Mwakilishi wa Wanawake wa Embu) na Kareke Mbiuki (Maara) na Mugambi Rindikiri (Buuri).

Katibu Mkuu wa Chama cha Jubilee Bw Jeremiah Kioni alipuuzilia mbali hatua hiyo akisema haina maana ‘na hakika huwezi kuwa Waziri ambaye ni msemaji wa kisiasa’.

Bw Kioni alisema ‘huu ni ujanja mwingine wa Rais Ruto anapotaka kututenganisha na kutulemaza kisiasa’.