Habari za Kitaifa

Korti yazima polisi kuvamia boma la Wanjigi

Na SAM KIPLAGAT September 11th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

POLISI wamezuiwa kuvamia au kuingia katika makazi ya mwanasiasa na mfanyabiashara Jimi Wanjigi mtaani Muthaiga, Nairobi wakisubiri uamuzi wa kesi iliyowasilishwa na mke wake, Irene Nzisa Wanjigi.

Jaji wa Mahakama Kuu, Joe Omido, vilevile ameagiza Kaimu Inspekta Jenerali wa Polisi Gilbert Masengeli au afisa yeyote anayefuata maagizo yake, kutochukua au kuharibu mali yoyote inayomilikiwa na familia ya Wanjigi kabla ya uamuzi kuhusu kesi hiyo kutolewa.

Bi Wanjigi na watoto wake walifika kortini wakiwashutumu polisi kwa kuvamia boma lao Agosti 8 ambapo wanadaiwa kuharibu mali yao na kuchukua vifaa kadhaa ikiwemo simu, pesa na bidhaa za thamani kama vile herini na pete za dhahabu.

“Kabla ya kesi kusikilizwa na kuamuliwa, korti imekubali kutoa agizo la kuwazuia washtakiwe au mtu yeyote anayefuata maagizo kutoka kwao, kutekeleza vitendo vyovyote vya kuwavamia walalamishi,” alisema Jaji Omido.

Jaji alimwagiza Bi Wanjigi kukabidhi nakala za kesi Bw Masengeli na Mkurugenzi wa Uchunguzi wa Uhalifu (DCI) Mohamed Amin, kabla ya tarehe ya kusikizwa kwa kesi hiyo, Septemba 24.

Bi Wanjigi amedai maafisa wa polisi walivamia makazi yenye yaliyopo Muthaiga mnamo Agosti 8, 2024 kabla ya kuingia boma lao kimabavu asubuhi iliyofuata.

Wakati wa uvamizi huo, alidai polisi walivunja lango la boma lao, wakavunja mlango na madirisha ya nyumba na kuharibu kamera za CCTV, vifaa vya kumulika na muziki.

Aidha, alidai maafisa walichukua simu tano, vifaa vya mawasiliano nyumbani, vipakatalishi tano, i-pad, na vinginevyo.

Alidai vilevile kuwa polisi walichukua pete na herini za thamani ya Sh3.6 milioni.

Polisi pia walidaiwa kutwaa pesa taslimu Sh51,600, herini za almasi zenye thamani ya Sh2.14 milioni miongoni mwa vifaa vingine.