Sonko amwokoa mwanachuo anayeshtakiwa kupanga kuchoma hoteli ya kifahari Nairobi
ALIYEKUWA Gavana wa Nairobi Mike Mbuvi Sonko amemlipia dhamana ya Sh5,000 mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Nairobi (UoN) aliyeshtakiwa kupanga kuteketeza hoteli ya kifahari ya Boulevard Hotel jijini Nairobi.
“Nimefika kortini kumlipia Bernard Wangila Ojiambo dhamana. Wanafunzi wenzake na watu wa familia wameniomba nimsadie kwa vile hawana uwezo wa kujimudu kifedha,” Bw Sonko alieleza mahakama.
Gavana huyu wa zamani wa Nairobi alisema “amemwonea huruma Ojiambo kwa vile anaendelea na mitihani akiwa mwaka wa nne chuo kikuu cha Nairobi na akikaa ndani atakosa kumaliza masomo yake.”
Bw Sonko alidokeza kwamba familia ya mshtakiwa inajizatiti kila iwezavyo kumsomesha na “amejitolea kumlipia dhamana katika moyo wa kusaidia wenye mahitaji.”
Bernard Wangila Ojiambo, alitiwa nguvuni na polisi Septemba 9,2024 kwenye barabara ya Harry Thuku akiwa na kipipa cha lita 5 kilichokuwa na petroli akiwa na wanafunzi wengine waliokuwa wanaandamana kupinga mfumo wa ufadhili wa elimu ya chuo kikuu.
Ojiambo alikana shtaka la kupanga kutekeleza uhalifu Septemba 9,2024.
Wakili Danstan Omari aliyemwakilisha Ojiambo aliomba aachiliwe kwa dhamana ya pesa kidogo akisema “anatoka familia maskini na dhamana ya juu itakuwa ni cheti cha kumfanya asalie rumande ya gerezani muda mrefu.”
Bw Omari aliomba hakimu mwandamizi Robinson Ondieki amwachilie mshtakiwa akafanye mtihani wake wa mwisho, kwa vile yuko mwaka wa 4 UoN.
Alipokana shtaka, kiongozi wa mashtaka Everlyne Mutisya alipinga maombi ya kuachiliwa kwa dhamana akisema “uchomaji wa shule na vyuo umekita mizizi na mshtakiwa akiwachiliwa atarudi kukamilisha nia yake.”
Akitoa uamuzi, Bw Ondieki alisema upande wa mashtaka haujawasilisha ushahidi wa kutosha kuwezesha mahakama kumnyima dhamana Ojiambo.
Bw Sonko alimlipia dhamana Ojiambo kisha akaachiliwa na kuenda nyumbani.
Awali, wakili Danstan Omari anayemwakilisha mshtakiwa alieleza mahakama petroli aliyoshikwa nayo Ojiambo ilikuwa ya pikipiki yake anayotumia kusafiri kutoka makazi yake hadi chuoni na “wala haikuwa ya kuchoma hoteli.”