Polisi: Watatu waliopigwa risasi Murang’a ni wahalifu waliokuwa wakitafutwa
IDARA ya Uchunguzi wa Jinai (DCI) imetoa maelezo mapya kuhusu wanaume watatu waliouawa kwa kupigwa risasi kwa njia isiyoeleweka mnamo Septemba 9 katika kijiji cha Mutoho, eneobunge la Kandara Kaunti ya Murang’a.
Watatu hao waliuawa kwa kupigwa risasi na wanaume waliokuwa kwenye magari mawili saa tatu usiku.
Huduma ya Kitaifa ya Polisi (NPS) inasema bado inachunguza tukio hili la mauaji.
Mauaji hayo yalijiri kukiwa na kilio cha kitaifa kuhusu maafisa wa polisi wanaoshukiwa kuhusika na mauaji ya kiholela, utekaji nyara na watu kutoweka.
‘Sasa tumepata maelezo muhimu kuhusu waathiriwa watatu wa mauaji ya Mutoho ikiwa ni pamoja na majina yao na walikoishi. Baada ya jamaa zao wa karibu kujitokeza ili kutambua mili hiyo, tunaweza sasa kufichua kuwa waliouawa ni Francis Maingi Mwaura, 39, Michael Kimando Maina, 36, na Kennedy Mwaura Mwangi, 27,” Mkuu wa DCI Murang’a Kusini Bw John Kanda alisema.
Aliongeza kuwa wote walikuwa wakaazi wa mtaa wa Kiandutu viungani mwa Mji wa Thika katika Kaunti ya Kiambu ‘na kwa bahati mbaya, wote walikuwa wakisakwa na maafisa wa usalama kwa kuhusika na uhalifu’.