Mapuuza ya serikali yageuza shule za bweni kuwa matanuri ya moto
SHULE za bweni nchini zimekuwa na historia ndefu na mbaya kuhusiana na mikasa ya moto.
Tukio la hivi karibuni katika Shule ya Msingi ya Hillside Endarasha Academy katika Kaunti ya Nyeri ambalo lilisababisha maafa ya wanafunzi 21, ni moja ya matukio mengi.
Huku nchi ikiendelea kuomboleza, shule zingine zimeripoti visa vya moto zikiwemo Shule ya Upili ya Wasichana ya Isiolo ambapo wanafunzi watatu walijeruhiwa; Shule ya Upili ya Njia, Meru; Shule ya Sekondari ya Bukhalarire, Busina; na Shule ya Upili ya Wavulana ya Isiolo.
Hakukuwa na visa vya maafa ya wanafunzi lakini uharibifu mkubwa ulishuhudiwa.
Mkasa wa Endarasha umefungua kurasa za kumbukumbu chungu kuhusiana na mioto shuleni ambao umejirudiarudia.
Umeibua haja ya kutilia mkazo zaidi utekelezaji wa miongozo ya usalama katika taasisi za elimu ambayo bila shaka imetelekezwa na wadau wa sekta ya elimu.
Miongoni mwa mikasa mibaya zaidi ni ule wa Shule ya Upili ya Kyanguli mwaka wa 2001 ambapo wanafunzi 67 waliangamia baada ya baadhi yawanafunzi kuteketeza bweni lao.
Matukio sawia yamejiri katika shule zingine nchini.
Mwaka wa 1988, kuliripotiwa maafa kutokana na moto katika Shule ya Upili ya Bombolulu.
Miaka mitatu baadaye, mkasa mwingine ulitokea katika Shule ya Upili ya St, Kizito, Meru, ambapo wanafunzi 19 walifariki huku wengine wakibakwa katika mkasa ambao uliyumbisha nchi.
Mnamo mwaka wa 1999, viranja wanne wa shule waliteketezwa katika Shule ya Upili ya Nyeri.
Wanafunzi wengine kumi walifariki motoni katika Shule ya Upili ya Moi Girls 2017 jijini Nairobi.
Licha ya hasara na maafa ya matukio haya, msururu wa moto unaoweza kuzuiwa unaendelea kuzonga shule nchini.
Aghalabu visa hivi hutokea usiku wakati wanafunzi hawana uwezo mkubwa wa kujiokoa.
Uchunguzi wa ajali hizi unadhihirisha mienendo ya mapuuza na utelekezaji wa miongozo ya usalama shuleni.
“Ni muhimu sana tuchukue hatua ya kukita sera na kanuni katika sheria ya nchi ili makosa yafafanuliwe vyema kikatiba,” alisema Msemaji wa Serikali, Dkt Isaac Mwaura wakati wa mkutano na waandishi wa habari Septemba 13, 2024.
“Wizara ya Elimu imeweka sheria na kanuni zinazoongoza viwango vya usalama shuleni, ikiwa ni pamoja na kuweka vizima-moto, idadi ya wanafunzi wanaolala katika bweni, kuwa na walezi au watu wazima katika kila bweni miongoni mwa mengine.”
Masharti haya, alibainisha, lazima yafuatwe kikamilifu ili kuwahakikishia wanafunzi wote usalama.
Ukaguzi wa 2020 ulibaini kuwa shule nyingi hazikuwa zimejiandaa vyema kwa dharura za moto kwa sababu hazikuwa na vifaa muhimu kama vile vizima-moto vilivyo katika hali nzuri pamoja na kengele ama ving’ora.
Ripoti hii ilinasa matokeo ya ripoti ya jopokazi la 2016 lililobuniwa baada ya wimbi kubwa la uchomaji wa shule na ghasia.
Chunguzi hizi zilihitimisha kuwa shule nyingi hazikuwa tayari kwa mikasa ya moto na kuwa miongozo ya usalama haikueleweka ama ilipuuzwa.
“Mkasa wa moto wa Endarasha unaonyesha changamoto za shule nchini kuhusiana na uwezo wa kuzuia moto na kufuata itifaki za mikakati ya dharura,” Dkt Mwaura alisema.
“Kenya haifai kushuhudia maafa ya watoto kwa sababu ya hitilafu za kimfumo. Kila shule inafaa kutekeleza kanuni za usalama na kuendeleza mafunzo ya kukabili moto.”
Baadhi ya shule zimejaribu kukita vifaa muhimu vya kudhibiti moto lakini wamekosa kuwa na majaribio ya mara kwa mara kujiandaa kwa mikasa kama hii.
Huko Hillside Endarasha, kwa mfano, ripoti zilifichua kwamba bweni lilikuwa na msongamano mkubwa, likiwa na wavulana 164 katika nafasi ambayo haikuundwa kubeba idadi kama hiyo.
Milango ya kutokea ilikuwa nyembamba, ikizuia uokoaji wa haraka wakati wa dharura.
Tukio hili la kusikitisha linaangazia hitaji la dharura la utekelezaji wa kanuni za usalama na miundombinu bora shuleni ili kuzuia majanga yajayo.
Mwongozo wa Kiwango cha Usalama wa 2008, ambao unatumika sasa shuleni, unaeleza hatua za usalama ambazo kila shule inapaswa kufuata.
Nafasi kati ya vitanda inapaswa kuwa angalau mita 1.2 na njia za shoroba ziwe mita mbili kwa upana.
Milango yote inapaswa kuwa na upana wa kutosha, angalau futi tano upana, na inafaa kufunguka kwa urahisi kwenda nje.
Hazipaswi kufungwa wakati wowote kutoka nje wakati wanafunzi wako ndani.
Mwongozo wa usalama unaelekeza wadau wa elimu kuzuru shule mara kwa mara ili kuimarisha usalama kwa kuhakikisha sheria inafuatwa.
Tafsiri na Labaan Shabaan