Makala

Ngeli ya Masengeli kudharau korti yamtupa gerezani

September 14th, 2024 4 min read

ALIKAIDI amri ya mahakama mara saba na sasa kilichobaki ni yeye kutumikia kifungo cha miezi 6 gerezani iwapo kufuata maelekezo ya mahakama ni kizungumkuti kwake Kaimu Inspekta Jenerali wa Polisi Gilbert Masengeli.

Ni kitendawili kwa afisa mkuu zaidi wa polisi akiwaza na kuwazua “ikiwa kwa muda wa miezi sita aliyofungwa bila faini, ataliwa na chawa pamoja na baadhi ya wafungwa aliowakamata na kuwatupa kizuizini.

Akiingia huko, watakula maharagwe pamoja, kulima mashamba ya serikali na kukamua maziwa ya ng’ombe wa serikali ambayo hawaruhusiwi kuyanywa hata wakiwa na hamu namna kiasi gani.

Ili kuhepa masaibu haya mnamo Alhamisi Septemba 12,2024, Bw Masengeli kupitia kwa wakili Cecil Miller aliwasilisha kesi kupinga kupitishwa kwa hukumu dhidi yake.

Bw Miller alijaribu kueleza mahakama kuwa Masengeli amekuwa na shughuli tele za kupanga masuala ya kiusalama na asiingefika kortini.

Jaji Mugambi alikataa kumsikiza Bw Miller aliyeungana na mawakili wa Serikali Emmanuel Mbitta na Wanjigu kumlilia Masengeli asipelekwe jela kunyolewa bila maji na kuvalishwa kunguru.

Mawakili waliowakilisha chama cha wanasheria nchini (LSK) Nelson Havi, Levi Munyeri walipinga ombi la Bw Masengeli wakizuia hukumu isisomwe wakisema “lazima kaimu IG Gilbert Masengeli asukumwe gerezani.”

Bw Havi alimsihi Jaji Mugambi asimame kidete na kulingana na kiapo cha ujaji kwamba ataitetea Katiba na kuhakikisha kila mwananchi amepata haki.

“Hakuna mtu aliye juu ya sheria hata kama anahudumu afisi ya juu zaidi nchini.

Lazima kila mmoja atii sheria,”Bw Munyeri aliambia Jaji Mugambi na kuongeza, “Lazima Masengeli ajue sheria ipo na haki za kila mwananchi zinatetewa na Katiba.”

Bw Munyeri alieleza mahakama kwamba kufikia sasa familia za ndugu wawili- Jamil Longton Hashim na Aslam Longton na mwanaharakati Bob Michemi Njagi- hazijui waliko.

Bw Munyeri alisema familia hizo hazijui ikiwa wako hai ama wameuawa. “Ni Masengeli tu anayeweza kueleza mahakama waliko watatu hao.”

Akitoa uamuzi Jaji Mugambi alimasukuma jela miezi sita bila faini.

Jisalimishe

Jaji huyo alimwamuru Masengeli ajisalamishe kwa Kamishna wa Magereza kuelezewa jela atakayohudumu.

Bw Masengeli ambaye Ijumaa (Septemba 13,2024) alikosa kufika kortini kwa mara ya nane alifungwa miezi sita bila faini na Jaji Lawrence Mugambi, kwa kudharau na kukaidi maagizo ya mahakama kuu mara saba.

Bw Masengeli alimtuma wakili Cecil Miller, mwenye tajriba ya juu, kufikisha kilio chake kwamba “hajadharau korti ila kamba za kazi na masuala ya kiusalama zimemfunga.”

Hata baada ya maelezo hayo Jaji Lawrence Mugambi alikataa kumsikiza Bw Miller na kusonga mbele kumuhukumu.

Hata hivyo Jaji Mugambi, aliahirisha kifungo hicho kianze baada ya siku saba.

“…ikiwa mfungwa huyu (Masengeli) atafika kortini katika muda wa siku saba kueleza kilichompata asitekeleze maagizo ya korti na kulia asisukumwe jela, huenda akapewa fursa. Vinginevyo, baada ya siku saba kumalizika, kifungo kitaanza.”

Jaji Mugambi aliamuru kwamba “endapo Masengeli hatajisalimisha kwa Kamishna wa Magereza kuelezewa gereza atakakotumikia kifungo hiki cha miezi sita, Waziri wa Usalama Prof Kithure Kindiki atahakikisha Masengeli ameingizwa jela kutumikia kifungo.”

Jaji Mugambi alisema, ikitiliwa maanani hakuna afisa wa polisi wa ngazi ya chini anayeweza kumkamata Bw Masengeli kumpeleka gerezani,Waziri wa Masuala ya Usalama Prof Kithure Kindiki, ndiye atakayehusika kuhakikisha ametumikia kifungo.

Kama angefika kortini Ijumaa baada ya hukumu kupitishwa, Masengeli angechukuliwa na askari jela kupelekwa gerezani moja kwa moja kuanza kutumikia kifungo kama wanavyofanyiwa wafungwa wengine.

Bw Miller alinyenyekea na kuomba fursa tu asikizwe lakini jitihada zake ziligonga mwamba huku mawakili wa LSK wakipinga vikali ombi hilo wakisema, “Leo Ijumaa ilikuwa siku ya kufungwa kwa Masengeli. Leo sio siku ya kujitetea na kusimulia hekaya. Alipewa muda mara saba kujiokoa lakini akakataa kufika kortini kueleza anayotaka kueleza sasa. Sharti aseme waliko ndugu hao na mwanaharakati.”

Bw Masengeli alijipata taabani alipokosa kufika kortini tangu Agosti 26,2024 kueleza waliko ndugu wawili- Jamil Longton Hashim na Aslam Longton na mwanaharakati Bob Michemi Njagi, wanaodaiwa walitekwa nyara na polisi Agosti 19, 2024, mjini Kitengela kaunti ya Kajiado.

“Katika kiapo changu sawia na kiapo cha Masengeli tulipoteuliwa kuwa Jaji na Kaimu IG tuliapa kuilinda Katiba na kuhakikisha kila mmoja amepata haki yake kwa mujibu wa sheria,” alisema Jaji Mugambi.

Alisema Bw Masengeli pia alikula kiapo cha kulinda maisha na mali, na kwamba lazima aeleze waliko ndugu hao wawili na Njagi, alioapa kulinda maisha yao na Wakenya wengine kwa mujibu wa sheria na Katiba.

“Kutofika kwake kortini ni kudharau mahakama, kukaidi Katiba na kuvunja sheria. Lazima kila mmoja nchini Kenya hata kama anahudumu katika wadhifa gani atii sheria na kuheshimu maagizo ya korti,” Jaji Mugambi alisisitiza akimsukuma jela Bw Masengeli.

Baada ya kupitisha hukumu hiyo Bw Miller aliomba mahakama imsikize Bw Masengeli pamoja na ombi la LSK kuhusu waliko watatu hao.

“Naomba mahakama isikize ombi na maelezo ya Bw Masengeli pamoja na ombi la LSK,” Bw Miller alimsihi Jaji Mugambi.

Bw Munyeri alisema tayari Bw Masengeli amefungwa na ikiwa hajaridhika na adhabu hiyo akate rufaa.

Jaji Mugambi aliamuru kesi hiyo itajwe mbele ya Jaji Enock Chacha Mwita anayesimamia kitengo cha uteteaji wa haki za binadamu mnamo Septemba 19,2024 kutoa mwelekeo atakayesikiza kesi hiyo kwa vile “atakuwa na kesi inayosikizwa na jopo la majaji watatu.”

Katika kesi ya LSK mahakama iliombwa imwamuru Bw Masengeli afike kortini kusema waliko ndugu hao wawili na mwanaharakati.

Chama cha LSK kinasema katika kesi hiyo kutoweka kwa watatu hao ni suala lililo na umuhimu mkuu kwa vile familia zao hazijui waliko.

LSK inaomba polisi wafikishe watatu hao kortini wakiwa hai au wakiwa maiti.

Wakiomba Bw Masengeli afike kortini LSK imesema sio tu ndugu hao na Njagi waliotoweka bali ni watu zaidi ya 20 waliotekwa nyara na watu wanaotuhumiwa kuwa polisi na hawajulikani waliko.

Awali Jaji Mugambi alimsamehe afisa mwingine mkuu Lazarus Opicho aliyewapigia simu dereva wake na mlinzi wake (wote ni maafisa wa polisi) akiwauliza aliko jaji huyo.

Aliomba msamaha akisema “hakuwa na nia mbaya ila alikuwa anataka kujua ikiwa wako salama pamoja na jaji baada ya kisa cha kupigwa risasi kwa hakimu wa mahakama ya Makadara, Monicah Kivuti Julai 2024.”

Monicah aliaga dunia

“Kama afisa mkuu wa kusimamia ulinzi wa maafisa wakuu serikalini niliwapigia simu dereva na mlinzi wako kujua ikiwa mko salama,” Bw Opicho alisema.

Lakini maelezo hayo hayakumridhisha Jaji Mugambi aliyemuuliza sababu ya kutompigia yeye mwenyewe badala ya kuwapigia dereva na mlinzi na “ana nambari ya simu ya jaji mwenyewe.”

“Sitarudia makosa hayo tena. Naomba msamaha,” Bw Opicho alirai.

Bw Opicho alisimama wima na kupiga saluti na kusema Thank you Sir (asante mkubwa).”

Aliondoka kortini kwa hatua za kasi.

[email protected]