Habari za Kitaifa

Wabunge kuamua ikiwa Kanja anafaa kuwa Inspekta Jenerali Mkuu wa Polisi

September 14th, 2024 2 min read

INSPEKTA Jenerali Mteule Douglas Kanja anatarajiwa kujua hatima yake Jumanne ijayo, Septemba 17, 2024 bunge la kitaifa litakapojadili ripoti iliyoandaliwa na kamati ya pamoja iliyomhoji kubaini ufaafu wake kwa wadhifa huo. 

Bunge hilo litarejelea vikao vyake vya kawaida baada ya likizo ya mwezi mmoja.

Tayari Seneti imeidhinisha uteuzi wa Bw Kanja kwa kuidhinisha ripoti hiyo iliyopendekeza ateuliwe rasmi kushikilia wadhifa huo.

Bw Kanja aliyependekezwa na Rais William Ruto kwa wadhifa huo kuchukua mahala pa Japhet Koome aliyejiuzulu, alipigwa msasa Agosti 14 na kamati ya pamoja ya bunge la kitaifa na seneti kuhusu usalama.

Kamati hiyo iliongozwa kwa pamoja na Mbunge wa Narok Magharibi Daniel Tongoyo na Seneta wa Baringo William Cheptumo.

Wabunge pia wanatarajiwa kuchambua ripoti ya Kamati ya Pamoja ya Bunge la Kitaifa na Seneti iliyompiga msasa mteule wa nafasi ya Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Ushindani David Kibet Kemei.

Kuhusiana na miswada inayohusu masuala ya bajeti, wabunge watashughulikia miswada miwili muhimu inayohusiana na ugavi wa fedha kati ya Serikali ya Kitaifa na serikali za kaunti.

Kwanza, wabunge watashughulikia Mswada wa marekebisho ya Sheria ya Ugavi wa Mapato ya 2024 unaolenga kupunguza viwango vya mgao wa mapato kati serikali ya kitaifa na serikali za kaunti.

Mswada huo uliandaliwa baada ya kukatiliwa kwa Mswada wa Fedha wa 2024 kufuatia maandamano ya vijana wa Gen Z mwezi Juni mwaka huu.

Bunge la kitaifa lilikuwa limeshughulikia mswada huo na kukubaliana na pendekezo lake kwamba mgao wa fedha kwa serikali za kaunti upunguzwe kutoka Sh400.5 bilioni hadi Sh380.5 bilioni.

Baada ya Mswada huo kushughulikiwa na Seneti, utarejeshwa kwa Bunge la Kitaifa ukiandamanishwa na marekebisho yaliyopendekezwa na maseneta au bila marekebisho yoyote.

Unatarajiwa kuwa na marekebisho baada ya idadi kubwa ya maseneta kupinga kupunguzwa kwa mgao wa fedha kwa kaunti kutoka Sh400.5 bilioni hadi Sh380.5 bilioni.

Magavana pia wameunga mkono msimamo wa maseneta wakidai kupunguzwa kwa mgao huo wa fedha kutaathiri shughuli za serikali za kaunti.