Kaunti zaweka rekodi bora kwa kukusanya mapato Sh58.95 bilioni
SERIKALI za kaunti ziliandikisha historia kwa kutimiza kiwango lengwa cha mapato zilizojikusanyia, tangu kuanza kwa ugatuzi, kwa kukusanya jumla ya Sh58.95 bilioni katika mwaka wa kifedha wa 2023/2024.
Kiwango hicho cha mapato kilitoka, kwa kiwango kikubwa, kwa sekta ya afya.
Kulingana na ripoti ya Msimamizi wa Bajeti (CoB) Margaret Nyakang’o sehemu kubwa ya mapato hayo ilitokana na ada za matumizi na matozo mengine katika vituo vya afya.
Pesa hizo hizo huhifadhiwa katika Hazina Maalum ya Kustawisha Vituo vya Afya (FIF).
Serikali za kaunti zinaweza kuwekeza pesa hizo moja kwa moja katika vituo vya afya kwa manufaa ya jamii lengwa.
Mapato yanayokusanywa na serikali za kaunti pia yameongezeka kutokana na kupanda kwa hitaji la huduma za afya katika kaunti zote 47.
Kando na hayo, kuanzishwa kwa mifumo ya ukusanyaji mapato kwa njia ya kieletroniki, katika kaunti nyingi nchini, kumechangia kuimarika kwa kiwango cha ukusanyaji ushuru.
Kuimarishwa kwa taratibu za ulipaji na ukusanyaji mapato kumezuia uwezekano wa kupotea kwa fedha na kuhakikisha kuwa wakwepaji ushuru wanalazimishwa kulipa.
Taasisi ya Bajeti Hub inasema kuimarishwa kwa kiwango ch ukusanyaji ushuru katika kaunti kumechangiwa, kwa kiwango fulani, na kupitishwa kwa Sheria ya Uboreshaji wa Vifaa vya 2023, inayolenga kuziwezesha vituo vya afya kutumia pesa zozote zinazokusanya kuimarisha vifaa katika taasisi hizo.
“Aidha, matumizi ya sehemu kubwa ya fedha zinazokusanywa yanahusiana na masuala ya afya pekee wala sio majukumu mengine,” akaeleza Afisa wa Mipango katika Bajeti Hub John Kinuthia.
Kulingana na ripoti ya Dkt Nyakang’o ya kati ya Julai 2023 hadi Juni 2024, Sh58.95 bilioni zilizokusanywa na sekali za kaunti zinawakilisha asilimia 72.8 ya kiwango cha mapato lengwa kila mwaka ya kima cha Sh80.94 bilioni.
Kiwango hicho cha mapato ambayo serikali za kaunti zilijikusanyia kinawakilisha ongezeko la asilimia 55.9 ikilinganishwa na Sh37.81 bilioni ambazo serikali hizo zilikusanya katika mwaka wa kifedha wa 2022/2023.
Serikali za kaunti ambazo zilipitishwa viwango vyao lengwa kwa mapato ni pamoja na kaunti ya Turkana iliyovuka kiwango chake lengwa kwa asilimia 241.2, Vihiga (asilimia 136.3), Kirinyaga (asilimia 118.4), Lamu (asilimia 116.2), Nandi (asilimia 113), Wajir (asilimia 110), Nyeri (asilimia 106.1), Samburu (asilimia 104.1) huku kaunti ya Muranga ikipitisha kiwango lengwa kwa asilimia 100.2.
Serikali za kaunti zilizoandikisha kiwango kidogo cha ukusanyaji mapato ni pamoja na Nyandarua iliyokusanya asilimia 42.1 ya kiwango lengwa, Machakos (asilimia 46.5), Mandera (asilimia 50.8), Nyamira (asilimia 53.8), Bungoma (asilimia 55.8), Kajiado (asilimia 56.1) huku Busia ikikusanya asilimia 56.9 ya kiwango lengwa cha mapato kwa mwaka.