Habari za Kitaifa

Wanasiasa wa UDA Ukambani walia Ruto amewasahau

Na PIUS MAUNDU September 15th, 2024 2 min read

VIONGOZI wa chama cha United Democratic Alliance (UDA) kutoka Ukambani, wameendelea kumkosoa Rais William Ruto wakidai ametenga eneo lao.

Aliyekuwa Mbunge wa Machakos Mjini Victor Munyaka, ambaye amekuwa mwandani wa karibu wa Rais William Ruto, sasa anamsuta kiongozi wa taifa kwa kuwatelekeza wandani wake katika eneo la Ukambani.

Kauli ya Dkt Munyaka imejiri wiki mbili baada ya aliyekuwa mwenyekiti wa Chama cha United Democratic Alliance (UDA) Johnson Muthama kudai Rais Ruto alibagua Ukamba wakati wa uteuzi wa maafisa wakuu katika serikali yake.

Akiongea katika hafla ya mazishi ya dadake, Rose Mwikali, Bw Munyaka alibadhiri kuwa huenda Dkt Ruto akapoteza uungwaji mkono katika kaunti za Kitui, Machakos na Makueni.

“Nyote mwafahamu kuwa nilirejelewa kama Kamotho wa Ukambani kutokana na uaminifu wangu kwa Ruto. Niliwaleta Mbunge wa Mwala Vincent Musyoka, Bw Muthama na Mbunge wa Kitui Mashariki Nimrod Mbai na kupitia bidii zetu eneo la Ukambani lilimpa Rais Ruto kura 250,000. Hizi ndizo kura zilizomwezesha kushinda urais.

“Namwambia rafiki yangu Rais Ruto akome kutenga Wakamba kwa sababu ya Munyaka, Kawaya, Mbai na Muthama ambao bidii yake ilimwezesha kupata ushindi. Tunashuhudia hali ambapo watu kutoka jamii ya Wakamba wanaoshikilia nyadhifa kuu serikalini wameanza kuzipoteza,” akasema katika eneo la Muthwani Kaunti ya Machakos, Ijumaa, Septemba 13, 2024.

Dkt Munyaka alitoa mfano wa aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kitaifa la Biashara Pamela Mutua, aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Kitaifa ya Nafaka na Mazao (NCPB) Joseph Kimote, aliyekuwa mwenyekiti wa Bodi ya Jumba la KICC Adelina Mwau, aliyekuwa kaimu afisa mkuu mtendaji wa Shirika la Usambaji Dawa Nchini (KEMSA) Andrew Mulwa na aliyekuwa kaimu Afisa Mkuu Mtendaji wa Mamlaka ya Kitaifa ya Kupambana na Pombe na Mihadarati (NACADA) John Muteti, kama miongoni mwa watu kutoka Ukambani waliopoteza vyeo vyao serikali majuzi.

Naibu Gavana wa Machakos Francis Mwangangi aliyehudhuria mazishi hayo aliwachekelea wandani wa Rais Ruto katika eneo la Ukambani kwa kuunga mkono utawala aliodai “umefeli Wakenya).

Alimtaka Dkt Munyaka kugura muungano wa Kenya Kwanza.