Hatari shirika la kukabiliana na ukame likisema halina pesa
MAMLAKA ya Kitaifa ya Kupambana na Ukame (NDMA) imeonya kuwa Wakenya watakabiliwa na hatari endapo kutatokea janga kwani imelemazwa kifedha kiasi cha kutoweza kushughulikia hali kama hiyo ya dharura.
Usimamizi wa mamlaka hiyo, ukiongozwa na Afisa Mkuu Mtendaji Hared Adan, uliwaambia wabunge Ijumaa, Septemba 13, 2024 kwamba awali walikuwa na hifadhi ya Sh2 bilioni za kukabiliana na majanga lakini mwaka huu wa kifedha wamesalia na Sh20 milioni tu za kugharamia shughuli zao zote.
NDMA ilisema kuwa ingawa imekuwa akiingilia kati kwa kuwasaidia waathiriwa wa majanga kama vile mafuriko, uvamizi wa nzige na kiangazi, wakati huo haina fedha za kushughulikia dharura kama hizo.
“Kwa kuwa mamlaka hii inayo matawi katika ngazi ya wilaya, huombwa kusaidia katika shughuli za ukusanyaji data na ushirikishi wa mikakati ya kukabiliana na majanga niliyotaja hapa na hata mkurupuko wa magonjwa yanayoathiri mifugo na binadamu, shughuli zinazohitaji pesa nyingi ambazo hatuna wakati kama huu,” akasema Bw Adan.
Afisa huyo aliwaambia wabunge wanachama wa Kamati ya Bunge la Kitaifa kuhusu Maendeleo ya Kanda kwamba bila usaidizi kutoka kwa wafadhili, hawawezi kuendesha majukumu yao.
Bw Adan aliiambia kamati hiyo kwamba NDMA inahitaji Sh60 milioni kushirikisha shughuli ya ukaguzi wa hali ya uwepo wa chakula, lakini imeweza kupata Sh30 milioni pekee kutoka kwa wadau huku serikali ikikosa kuitengea mgao wa bajeti.
Ukaguzi wa hali ya uwepo wa chakula ni muhimu kwa sababu huisaidia serikali kufanya maamuzi ya kutafuta fedha na rasilimali nyinginezo kukabiliana na baa la njaa.
“NDMA haina mgao wa bajeti kutoka kwa serikali kwa ajili ya kushirikisha mikakati ya kupambana na kiangazi, ilhali hiyo ndio wajibu wake mkuu. Tunahitaji Sh90 milioni kwa mwaka kuendesha shughuli hii, pesa ambazo hatuna wakati huu,” Bw Adan akaiambia kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge wa Kipipiri Wanjiku Muhia.