Masengeli kukata rufaa hukumu ya kurushwa jela akidai anaandamwa kisiasa
KAIMU Inspekta Jenerali wa Polisi Gilbert Masengeli anapanga kukata rufaa hukumu iliyomsukuma jela miezi sita kwa kudharau la maagizo ya mahakama, mmoja wa mawakili wake amesema.
Hukumu ya kumtupa jela mkuu huyo wa polisi, ilitolewa Ijumaa, Septemba 13, 2024 na Jaji Lawrence Mugambi wa Mahakama Kuu baada ya afisa huyo kukosa kufika mahakamani mara nane jinsi alivyoagizwa.
Bw Masengeli alitakiwa kufika mahakamani binafsi ili kutoa maelezo ya ni wapi waliko wanaharakati watatu ambao wanaaminika kutekwa nyara na maafisa wa polisi mnamo Agosti 19, 2024, mjini Kitengela, Kaunti ya Kajiado.
Lakini mkuu huyo wa polisi alipuuza maagizo hayo na hajawahi kukanyaga mahakamani kueleza waliko ndugu wawili- Jamil Longton Hashim na Aslam Longton na mwanaharakati Bob Michemi Njagi.
Akihutubia wanahabari mjini Nyamira mnamo Jumamosi, Septemba 14, 2024, mmoja wa mawakili wa Bw Masengeli, Danstan Omari alisema yeye na mawakili wenza wataelekea mahakamani Jumatatu ijayo, Septemba 16, 2024 kupinga hukumu aliyopewa mteja wao.
Wakili huyo alisema kuwa mteja wao alikuwa akipigwa vita vya kisiasa na watu fulani ambao hakuwataja na kusema hayo yanachochewa na mchakato wa kutafuta atakayechukua nafasi ya Inspekta Jenerali kufuatia kujiuzulu kwa Japhet Koome.
“Tunajua kwamba nafasi ya Inspekta Jenerali wa Polisi i wazi na harakati za kumtafuta atakayechukua nafasi hiyo inaendelea. Yule aliyeteuliwa kwa nafasi hiyo, Bw Douglas Kanja ana viunzi ambavyo ni sharti aviruke ndipo apewe kiti hicho. Amekwisha idhinishwa na Bunge la Seneti na sasa amebakisha lile la kitaifa,” akasema Wakili Omari.
“Lakini tunajua kuwa, kuna suala zito linalomkodolea macho Bw Kanja kwani kuna uwezekano akakosa kuidhinishwa kwa kuwa anatoka eneo moja na Mkuu wa Majeshi Charles Kahariri. Huenda akatemwa kufuatia kigezo hiki ikiwa Bunge la Kitaifa litatilia maanani usawa wa kimaeneo. Na ikiwa hilo litatokea, basi Bw Masengeli atakuwa kwenye nafasi nzuri kuteuliwa katika wadhifa huo kwani anatoka eneo la Magharibi mwa Kenya. Ili kumpaka matope, watu hao wanataka kumsawiri Masengeli kama mtu asiyetii mahakama ilhali ni mtiifu,” Omari alisema.
Kulingana na wakili huyo, watakapoelekea mahakamani kukata rufaa, wataomba uamuzi wa jaji Mugambi uwekwe kando.
Wakili huyo aliyebobea masuala ya sheria alitumia fursa hiyo kummiminia sifa mteja wake akisema alipaa ngazi kuanzia afisa wa chini hadi sasa ambapo yeye ni kaimu Inspekta Jenerali wa polisi na mmoja wa manaibu wa Inspekta Jenerali.
Kwa kuwa hakuna afisa yeyote wa ngazi ya chini anayeweza kumkamata Bw Masengeli, Jaji Mugambi alimtwika Waziri wa Usalama wa Ndani Profesa Kithure Kindiki jukumu la kuhakikisha Masengeli amesukumwa korokoroni kula maharagwe pamoja na wafungwa wengine.
Lakini wakili Omari alihoji kuwa Profesa Kindiki hana mamlaka ya kukamata watu.
Alisema agizo la kutaka Bw Masengeli afungwe jela halitawezekana na litazama maji jinsi ilivyotokea wakati wa aliyekuwa Mkuu wa Kitengo cha Masuala ya Uhalifu wa Makosa ya Jinai (DCI) George Kinoti.
Mnano Novemba 2021, Bw Kinoti alipewa kifungo cha miezi minne gerezani baada ya kukiuka agizo la mahakama la kumtaka amrudishie mfanyabiashara mwanasiasa Jimi Wanjigi bunduki zake.