• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
REKODI YA GUINNESS: Hajanyoa nywele kwa miaka 33 ili apate umaarufu

REKODI YA GUINNESS: Hajanyoa nywele kwa miaka 33 ili apate umaarufu

Na CHARLES WANYORO

MWANAUME ambaye hajanyoa nywele zake kwa muda wa miaka 33 yuko mbioni kuvunja rekodi kuwa mtu aliye na nywele ndefu zaidi ndefu zaidi nchini Kenya.

William Kaimenyi Rimberia, 59, mkazi wa kijiji cha Kambakia, Kaunti ya Meru aliacha kunyoa nywele na ndevu zake kama njia mojawapo ya kuunga mkono harakati za kupigania mfumo wa vyama vingi nchini. Mashungi yake ya nywele na ndevu sasa yamekuwa magumu na imara na yamefikia urefu wa mita moja.

Baada ya kufutiliwa mbali kwa kifungu cha sheria 2(a) kilichopiga marufuku mfumo wa vyama vingi mnamo Desemba 1991, Bw Kaimenyi aliamua kuendelea kutonyoa nywele zake na ndevu.

Anasema kuwa nywele ndefu, ambazo kwa kawaida huhusishwa na mashujaa wa Maumau, humfanya kuwa na na ujasiri wa kuendelea kupigania haki mbalimbali za kibinadamu.

“Lengo langu lilikuwa kunyoa baada ya mfumo wa vyama vingi kuhalalishwa. Baadaye niliamua kuendelea kukuza nywele na ndevu kama ishara ya ukombozi wa pili,” akasema.

Bw Kaimenyi ambaye ni mwanachama wa baraza la wazee wa jamii ya Wameru la Njuri Ncheke, amekuwa akipigania haki za wajane na watu wengine wanaodhulumiwa kutoka kijiji kimoja hadi kingine.

“Watu wengi wanakumbana na dhuluma mbalimbali hata leo. Kwa mfanoninafuatilia kesi ya mjane ambaye shamba lake lilinyakuliwa na kanisa mjini Maua. Mjane huyo alipata agizo la mahakama la kutaka kanisa hilo libomolewe mnamo 2014 lakini kufikia sasa hakuna hatua ambayo imechukuliwa,” akasema.

Licha ya kuwa mwanaharakati, Bw Kaimenyi anasema kuwa kufikia sasa hajapata fursa ya kuanzisha familia yake mwenyewe. Alisema nywele zake ndefu ni kivutio kikuu kwa wakazi wa eneo hilo ambao husimama na kumpiga picha wanapokutana naye.

Miaka michache iliyopita watu wenye nywele ndefu walihusishwa na kundi haramu la Mungiki. Lakini Bw Kaimenyi anasema kuwa hajawahi kuhangaishwa na yeyote kwa ‘kufuga’ nywele ndefu.

“Watu hunisimamisha njiani na kuanza kutamani nywele zangu. Kuna wakati nilienda katika Mahakama ya Juu kushughulikia kesi fulani na kila nilipopita watu walibaki na mshangao.

“Nywele zangu ni kivutio kikubwa kwa watu na ninafurahia kuwa nazo na wala haziniumizi ninapolala usiku,” akasema Bw Kaimenyi.

You can share this post!

Hisia mseto kuhusu pendekezo la kuunganisha kampuni za miwa

Oparanya abwaga wanne kuongoza kundi la magavana

adminleo