Akili MaliMakala

Himizo wafugaji wajiundie malisho  

Na SAMMY WAWERU September 17th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

BEI ya malisho ya mifugo ya madukani ikiendelea kuwa ghali, wakulima wamehimizwa kukumbatia mifumo ya kujiundia. 

Kulingana na wataalamu, hatua hiyo itawasaidia kushusha gharama kwa kiwango kikubwa.

Hata hivyo, wanapaswa kuwa na chanzo cha kuaminika cha malighafi na fomula maalum.

“Kwa wanaoendeleza ufugaji-biashara, kupata faida lazima watambue njia mbadala kupunguza gharama. Kujiundia chakula ni mojawapo ya mbinu hizo,” anashauri Dkt Maurice Msanya, mtaalamu wa mifugo na vetinari kutoka kampuni ya Bimeda.

Dkt Maurice Msanya akizungumza katika Kongamano la Amagoh Dorper Stud, Nairobi. PICHA|SAMMY WAWERU

Dkt Msanya vilevile ni Meneja wa Mauzo na Soko katika kampuni hiyo.

Anakiri bei ya juu ya chakula cha mifugo cha madukani ni kati ya changamoto zinazohangaisha wakulima nchini.

Gharama ya malisho imekuwa ikipanda, hasa Kenya ilipokumbwa na janga la Covid-19 mwaka wa 2020.

Miaka mitatu baadaye, hata hivyo, ulimwengu ulitangazwa kuwa huru dhidi ya virusi vya corona.

Bei ya malighafi ya chakula cha mifugo inazidi kuwa ghali, muungano wa viwanda vya utengenezaji chakula cha mifugo nchini (Akefema) ukikadiria kampuni 37 kufunga milango kufikia 2022.

Dkt Maurice Msanya, mtaalamu wa mifugo na vetinari kutoka kampuni ya Bimeda akishauri wafugaji kuhusu matunzo ya kondoo. PICHA | SAMMY WAWERU

Malighafi yenye virutubisho vya Protini hasa ndiyo bei ghali mno, ikikadiriwa Kenya huagiza kutoka nje ya nchi zaidi ya asilimia 80 ya malighafi yanayotumika kutengeza malisho ya mifugo.

Ushuru wa ziada (VAT) na kodi zinazotozwa zimetajwa kuchangia hali kuwa mbaya.