Ufugaji kondoo aina ya Dorper unavyompa hela kibao
ENEO la Kantafu, kilomita 50 hivi kutoka Jiji la Nairobi, ni mradi wa kondoo wa Bernard Njaramba.
Bernard, ni mwasisi wa Amagoh Dorper Stud, mfugaji hodari wa kondoo aina ya Dorper.
Aina hiyo ya kondoo kutoka nchi ya Afrika Kusini, ni chotara (crossbreed) kati ya Dorset Horn na bridi yenye kichwa cheusi kutoka Persian.
Unapozuru mradi wa Bernard, utakaribishwa na mseto wa sauti za kondoo zinazohinikiza mazingira.
Anakiri, anaposkia sauti hizo humfanya kutabasamu.
“Kila sauti, ninaweza kukueleza inachomaanisha. Kwa mfano, unayoskia sasa ni ‘kilio’ cha furaha,” akaambia Akilimali Dijitali wakati wa ziara katika mradi wake ulioko kilomita chache kutoka kituo cha kibiashara cha Malaa.
Mradi huo umekalia kwenye shamba la ukubwa wa ekari 40.
Akiwa alilelewa katika familia iliyoenzi ufugaji, Bernard aliingilia ufugaji kondoo 2011.
Mifugo wangu wa kwanza walikuwa ng’ombe, kisha baadaye nikazamia mbuzi na kondoo, anasema.
Hatimaye, aliishia kuondoa mbuzi kwenye mahesabu, akasalia na kondoo wa Dorper.
Anasema, chocheo hilo lilitokana na mapenzi yake kwa kondoo hao wa kisasa wa nyama.
Dorper wanasifiwa kutokana na hulka za nyama zake zilizoingiana na kusawazishana na mafuta.
Bernard anafichua kwamba alianza na kondoo watano pekee, na muda ulivyozidi kusonga mradi wake ukapanuka.
“Nilianza mdogo mdogo, na huo ndio ushauri wangu kwa wenye ari kufanya kilimo-ufugaji-biashara,” asema.
Miaka 12 baadaye, Amagoh Dorper Stud inajivumia kuwa na idadi ya Dorper wasiopungua 500.
Mazizi ya mifugo hao yametengenezwa kwa muundo wa kisasa, kiasi cha kuwa na vyumba vya malazi.
Yamegawanywa kwa msingi wa umri, jinsia na vilevile kuna makao maalum ya wana wa kondoo hao.
Bernard anawasifu akisema wanapotoka malishoni hujipeleka kwenye vyumba vyao vya mapumziko na kulala.
Dorper, ni kondoo walioimarishwa, na wana uwezo kuhimili athari au mikumbo ya maeneo kame (ASAL) na maeneo yenye baridi.
Kulingana na Phil Rawlins, mtaalamu wa Dorper kutoka Afrika Kusini anayefahamika katika ngazi za kimataifa, kondoo hao wa rangi nyeupe na kichwa cheusi, maumbile yake yanawawezesha kustahimili athari za mabadiliko ya tabianchi kama vile ukame na kiangazi.
“Mahitaji yake ya lishe ni ya chini, na hugeuza chakula upesi kuwa nyama,” Rawlins anadokeza.
Hulka hizo, zinafanya Dorper kuwa mifugo bora zaidi wa nyama.
Isitoshe, kondoo mama ana malezi ya kiwango cha juu.
Aidha, hukomaa upesi kugeuzwa kuwa kitoweo – kati ya miezi sita na minane chini ya matunzo bora na faafu.
Wale wa kike, kwa muda wa mwaka mmoja baada ya kuzaliwa huwa tayari kutungishwa ujaujizito, na Bernard huwafuga kwa wingi kwa minajili ya biashara ya uzalishaji.
Bei huchezea kati ya Sh45, 000 hadi Sh100, 000, kulingana na umri na vigezo anavyoweka.
Amagoh Dorper Stud ni kituo cha mafunzo ya kondoo hao wa kisasa, na Julai 2024 mradi huo uliandaa kongamano la mafunzo, makala ya pili.
Alipoulizwa jinsi amefanikisha ufugaji wa Dorper, Bernard alisema kando na kuwa na mapenzi ya dhati kwa wanyama hao, mfugaji anapaswa kuhakikisha anapata bridi bora.
Mfugaji huyu hujiundia malisho ya kondoo wake, ambapo ana mashine ya shughuli hiyo.
Aghalabu, huboresha bridi zake kwa kununua wa kuzalisha kutoka Afrika Kusini.
Mitandao ya kijamii kama vile Facebook na Tiktok, ndiyo majukwaa yake kuvumisha soko.