Habari za Kitaifa

Nyong’o ataka wafuasi na viongozi wa ODM waseme Ruto tosha

Na JUSTUS OCHIENG’ September 18th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

KIONGOZI wa ODM Profesa Anyang’ Nyongó amewataka viongozi na wanachama wote waunge mkono Serikali Jumuishi inayoongozwa na Rais William Ruto huku mgawanyiko ukiendelea kushuhudiwa chamani kuhusu suala hilo.

Wiki iliyopita, Prof Nyong’o aliteuliwa Kaimu Kiongozi wa ODM na Kamati Simamizi ya Chama (CMC).

Ameonekana kuanza kwa makeke akisema chama kinamakinikia ushirikiano na serikali kwa ajili ya maendeleo.

Mnamo Jumanne, Rais Ruto aliongoza mkutano wa kwanza wa mawaziri ndani ya serikali jumuishi ambao uliwashirikisha mawaziri watano kutoka ODM.

Katika mahojiano na Taifa Leo, Prof Nyongó ambaye pia ni Gavana wa Kisumu, alisema ODM inamakinikia uwepo wa taifa moja lililoungana.

“ODM inamakinia uundaji wa serikali ya kitaifa inayozingatia demokrasia na maendeleo ili Kenya ibadilike. Serikali ambayo kuna hakikisho la usawa na ustawi wa kijamii,” akasema Prof Nyongó.

ODM ilianza ushirikiano na utawala wa sasa baada ya maandamano kuchacha nchini, vijana wakipinga Mswada wa Fedha 2024 ambao ulikuwa na mapendekezo mengi ya ushuru.

Baadhi ya wanachama wa ODM kwa sasa wapo katika njiapanda, wasijue waunge serikali au wasalie upinzani, baada ya ushirikiano huo kuanza.

Hii ni kwa sababu Rais Ruto na utawala wake, nao umesisitiza kuwa utaendesha kampeni kali kuhakikisha Raila Odinga anawahi uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC).

Kwa sasa kumeibuka mirengo miwili ndani ya chama, ambapo mmoja unaunga ushirikiano na serikali na mwingine ukipinga.

Wanaounga ni Seneta wa Siaya Dkt Oburu Oginga, Kiongozi wa Wachache Junet Mohamed, Mwenyekiti wa ODM Gladys Wanga, Gavana wa Kisii Simba Arati, Mbunge wa Makadara George Aladwa na Mwekahazina Timothy Bosire.

Mrengo unaopinga ni Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna, Ruth Odinga, dadake Raila na Mbunge Mwakilishi wa Kaunti ya Kisumu, Babu Owino (Embakasi), Gavana wa Siaya James Orengo na wabunge Nabii Nabwera (Lugari) na Caleb Amisi (Saboti).

Mgawanyiko huo ndio ulisababisha baadhi ya wabunge wa ODM wiki jana wasusie mwaliko wa kujiunga na Rais Ruto, kwenye ziara yake eneo la Kibra.

Pia walikataa mwaliko wa kujiunga na Rais kwenye mkutano uliofanyika ikulu.

Prof Nyongó alitetea kujumuishwa kwa baadhi ya wanachama wao kwenye baraza la mawaziri, akisema hatua hiyo ilikuwa ikilenga kuunganisha nchi.

“Kwa kuwa na baadhi ya wanachama wetu kwenye Baraza la Mawaziri la UDA, tunawataka wapanue maono ya serikali ili Kenya ionekane kama taifa moja.

“Kupitia hii, hali ya baadaye ya taifa itafanikishwa na kuimarishwa kwa demokrasia na maendeleo,” akasema.

Dkt Oginga na Bw Mohamed nao wameashiria kuwa huenda ODM itakuwa na muungano wa kisiasa na Rais Ruto mnamo 2027 mradi tu atimize ahadi alizotoa kwa Wakenya.

Bw Mohamed naye amemtaka Rais ahakikishe kuwa Raila anafanikiwa AUC huku Dkt Oginga akisema wanataka kurudisha mkono uungwaji mkono ambao Rais alitoa kwa Raila mnamo 2007.