Habari za Kaunti

Hofu magenge yakivamia watu hadharani jijini Mombasa

Na WINNIE ATIENO September 18th, 2024 2 min read

KATIKA kipindi cha miezi miwili hivi, wakazi wa Mombasa wameshuhudia ongezeko la uhalifu katikati mwa jiji hilo la kitalii huku wasiwasi ukiendelea kutanda kuhusu hali ya usalama.

Hii ni baada ya magenge ya vijana wenye silaha butu wanaotumia pikipiki kuvamia wakazi mchana peupe.

Vijana hao wahalifu hujifanya wanapelekea wateja mbalimbali mizigo huku wakiotea watu wanaoongea kwa simu katikati mwa mji na wale wanaotoka maduka makuu kununua bidhaa na kuwapokonya mali zao huku wakiwatishia kwa panga.

Sehemu hatari zaidi ni pamoja na maduka makuu, barabara za Haile Selassie, Digo, Moi, Jomo Kenyatta na Dedan Kimathi.

Baadhi yao wamenaswa kwenye kamera za CCTV namna wanavyotumia pikipiki kuibia wakazi wakijifanya wanasafirisha mizigo.

Wadau wa sekta ya utalii, wakiongozwa na Mwenyekiti wa Chama cha Utalii cha Pwani ya Kenya (KCTA), Bw Victor Shitakha, wametaja magenge hayo kuwa hatari kwa biashara jijini.

“Usalama umedorora Mombasa, tunashukuru kwamba hakuna mtalii ambaye ameshambuliwa lakini kama wakazi tunaishi na uoga sana. Siku hizi watu hata wanaogopa kwenda jijini,” alisema Bw Shitakha.

Alisihi serikali ya kitaifa na ile ya kaunti kushirikiana na kuwatafutia vijana wa Mombasa ajira badala ya kukaa maskani.

Kamishna wa Kaunti ya Mombasa, Bw Mahmood Noor, alisema maafisa wa usalama tayari wanashughulikia suala hilo na kuweka mikakati ya kukabiliana na magenge hayo.

Aliwahakikishia wakazi kwamba doria za usalama zimeimarishwa jijini na polisi wanasaka magenge ya wahalifu wanaotekeleza uharibifu.

Bw Noor aliongeza kuwa operesheni ya usalama ambayo ilianzishwa siku chache zilizopita tayari imesaidia washukiwa kadha kunaswa ambao watachukuliwa hatua za kisheria.

Operesheni hiyo ilianza takribani wiki mbili zilizopita, ilipozinduliwa na Kaimu Inspekta Mkuu Gilbert Masengeli na Mkurugenzi wa Idara ya Upelelezi wa Uhalifu (DCI), Mohamed Amin ili kukabiliana na uhalifu Mombasa.

“Tutaongeza operesheni zaidi, lazima tudhibiti ukosefu wa usalama. Lazima tuhakikishe usalama umeimarishwa. Lakini wanyang’anyaji wengi wamekamatwa; wale ambao bado hawajakamatwa wanachunguzwa,” aliongeza mkuu huyo wa polisi.

Bw Masengeli aliwataka wananchi kutoa taarifa kwa polisi zitakazofanikisha kukamatwa kwa wahalifu hao.

Serikali ya Kaunti ya Mombasa ilianza kuondoa familia za kurandaranda mitaani, ikisema ongezeko lao pia limechangia ukosefu wa usalama jijini.

Afisa mkuu wa masuala ya uongozi wa mitaa katika kaunti, Bw Abdala Daleno, alisema serikali ya kaunti ikiongozwa na Gavana Abdulswamad Nassir haitavumilia ukosefu wa usalama.

“Watoto na vijana ambao wanatumia mihadarati wanapelekwa katika vituo vya kurekebishia tabia,” aliongeza.

Bw Daleno alisema wanashirikiana na maafisa wa polisi kwenye zoezi hilo.Kulingana naye, baadhi ya watu wanaorandaranda mitaani wamebainika kuwa raia wa kigeni kutoka nchi jirani kama vile Tanzania.