Habari za Kitaifa

Mtaalamu ashauri serikali jinsi ya kufadhili elimu vyuoni bila kufinya wananchi

Na LAWRENCE ONGARO September 18th, 2024 1 min read

SERIKALI imehimizwa kutafuta njia mwafaka ya kupata fedha kwa ajili ya bodi ya mikopo ya elimu ya vyuo (HELB ).
Naibu Chansela wa Chuo Kikuu cha Mount Kenya Dkt Vincent Gaitho, alisema jambo hilo litanufaisha wanafunzi wengi ambao hawana uwezo wa kupokea fedha za mkopo wa HELB.
Alipendekeza  serikali kutumia fedha kutoka kwa hazina ya mamlaka ya kuhifadhi mali  zisizodaiwa ambazo zimefika kiwango cha Sh 45 bilioni.
“Fedha hizo zaweza kutumiwa kwa HELB halafu zirejeshwe baadaye,” alisema Dkt Gaitho.
Dkt Gaitho ambaye ni mwenyekiti wa bodi ya muungano wa sekta ya elimu ya shule za Kibinafsi (KEPSA), alitoa pendekezo hilo akiwa katika Chuo cha Machakos.
Alisema kwa siku za hivi karibuni mbinu za kutoa fedha za HELB zimekashifiwa na wazazi wakidai ya kwamba fedha hizo hucheleweshwa huku kukiwa na mapendeleo.
Wakati huo pia alitoa wito kwa mashirika makubwa nchini, kujitokeza kuchanga fedha kama njia ya kuisaidia jamii na kuelekeza fedha hizo kwa mikopo ya HELB.
Chansela huyo pia alipendekeza kuwa mali ya ufisadi ya  Sh 5 bilioni zilizotwaliwa na mamlaka ya ufisadi (EACC) hivi majuzi ziwasilishwe kwa serikali ili kusaidia  katika mikopo ya wanafunzi.
Alieleza kuwa fedha zilizokopeshwa wanafunzi katika vyuo vya kibinafsi zilipunguzwa kutoka Sh 70,000 hadi Sh 40,000.
Mbunge wa Dagoretti Kaskazini alipendekeza kuwa fedha zote za basari zilizotumika kutoka serikali kuu na za kaunti, mashirika ya serikali na ya kibinafsi yajumuishwe katika kapu moja, katika mikopo ya elimu.
Alitoa wito kwa HELB kurahisisha mikopo kwa wanafunzi wote wanaohitaji fedha hizo.
Alipendekeza kuwa wanafunzi wa vyuo vikuu wasio na vitambulisho vya kitaifa wakubaliwe kutumia vyeti vya kuzaliwa ama nambari ya usajili kwa ajili ya mitihani ya kitaifa ya sekondari – KCSE Index Number.
Makamu Chansela wa Chuo kikuu cha Machakos Prof James Mwola alisema kuwa wakati huu wanatarajia kupokea wanafunzi wa mwaka wa kwanza wapatao 3,000 huku asilimia 80 wakiwa tayari wamesajiliwa chuoni.