Kanja kuapishwa kuwa Inspekta Jenerali wa Polisi
INSPEKTA Jenerali Mteule Douglas Kanja anatarajiwa kuapishwa rasmi wakati wowote kuanzia Alhamisi baada ya Bunge la Kitaifa kuidhinisha uteuzi wake Jumatano.
Hii ni baada ya wabunge kupiga kura ya kuunga mkono ripoti ya kamati ya pamoja ya Bunge la Kitaifa na Seneti iliyopendekeza uteuzi wa Bw Kanja uhalalishwe.
“Kwa hivyo, Bunge hili limeidhinisha uteuzi wa Douglas Kanja kuwa Inspekta Jenerali wa Polisi wa Jamhuri ya Kenya,” akasema Spika Moses Wetang’ula.
Wabunge walipitisha ripoti hiyo baada ya kumaliza kuijadili tangu Jumanne, mjadala huo ulipoanzishwa na mwenyeti wa Kamati ya Bunge kuhusu Usalama Gabriel Tongoyo.
Wakati wa mjadala huo, wabunge wa mirengo ya Kenya Kwanza na Azimio la Umoja-One Kenya walimsifia Bw Kanja wakimtaja kama afisi mwadilifu na mwenye tajriba pamoja ikizingatiwa kuwa amehudumu katika idara ya polisi kwa miaka 39.
“Bw Kanja ni afisa ambaye amafanya kazi yake kwa bidii na uadilifu mkubwa. Hii ndio maana amehudumu kwa miaka 30 katika Huduma ya Kitaifa ya Polisi (NPS) na hajawahi kutajwa katika sakata yoyote ya ufisadi au kuhusishwa na vitendo vya ukiukaji wa sheria na kanuni za utendakazi wa polisi. Hii ndio maana kamati hii haikumpata na dosari yoyote ilipompiga msasa Agosti 18,” Bw Tongoyo akasema.
“Kwa hivyo, kamati ya pamoja ya bunge hilo na seneti inawaomba wabunge wapitishe uteuzi wake ili awahudumie Wakenya katika wadhifa huu muhimu,” Mbunge huyu wa Narok Magharibi akasema.
Baada ya kuapishwa, Bw Kanja atachukua rasmi nafasi iliyosalia wazi kufuatia kujiuzulu kwa Japhet Koome mnamo Julai 24, 2024.