Habari za Kitaifa

Hatari kwa usalama magaidi wakijifanya wanariadha Kenya

Na TITUS OMINDE September 19th, 2024 2 min read

KITENGO cha Polisi cha Kukabili Ugaidi (ATPU) kimeimarisha msako dhidi ya wahamiaji haramu wanaojifanya wanariadha wa kimataifa katika kambi za mazoezi mjini Iten.

Takwimu kutoka Mahakama ya Eldoret na Iten zinaonyesha kuwa angalau wageni wawili wanafikishwa mahakamani kila mwezi kwa kushukiwa kuwa magaidi na kuwa nchini kinyume cha sheria.

Wengi wa washukiwa hao hujifanya kuwa wanariadha wa kimataifa wanaofanya mazoezi Iten au watalii wanaozuru eneo hilo, hata hivyo vyeti vyao vya kusafiria huwa havionyeshi kuwa ni wanariadha.

‘Visa vya washukiwa wanaokamatwa Iten wakijifanya wanariadha wa kimataifa vinatia wasiwasi, wanariadha wanafaa kuweka miundo ifaayo ili kuhakikisha kuwa wageni hawajiungi nao kwa kisingizio cha kuwa wanariadha,’ alisema afisa mmoja mkuu kutoka ATPU jijini Eldoret.

Afisa huyo kutoka ATPU ambaye hakutaka kutajwa jina alisema baadhi ya washukiwa hao hutumia muda wao mwingi kupiga picha majengo ya kifahari jijini Eldoret na kuibua hisia mseto kuhusu shughuli zao nchini,” afisa huyo.

Wiki hii washukiwa wawili akiwemo raia wa Pakistani na mwingine kutoka China walifikishwa mbele ya Hakimu Mkuu wa Eldoret kwa tuhuma za kuwa majasusi wa ugaidi nchini.

Younas Usman raia wa Pakistan alizuiliwa kwa siku nne akisubiri uchunguzi kufanywa na ATPU kubaini shughuli zake nchini baada ya kukamatwa na ATPU jijini Eldoret ambapo alidai kuwa mwanariadha anayefanya mazoezi katika eneo hilo.

Akiwasilisha ombi la kumzuilia huku uchunguzi ukiendelea, afisa wa uchunguzi Phanuel Kaaria kutoka ATPU alisema mshukiwa alikamatwa katika jiji la Eldoret akijihusisha na biashara ya kuuza simu.

Bw Kaaria aliambia mahakama kuwa jibu hilo halikueleza sababu za msingi zake kuwa nchini na hivyo kuibua tuhuma za kuwa gaidi.

Aidha aliambia mahakama kuwa alitaka muda zaidi wa kuchunguza jinsi alivyoingia nchini na alichokuwa akifanya katika jji la Eldoret.

Mnamo Septemba 2023, mwanariadha wa New Zealand alikamatwa mjini Iten baada ya kupatikana na bunduki bila leseni.

Polisi waligundua bunduki hiyo wakati wa kukamatwa kwa mshukiwa baada ya kushtakiwa kwa unyanyasaji wa kijinsia.